Na Francis Godwin
ASKOFU wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa Dkt.Owdenburg Mdegela amewapongeza waumini wa Dayosisi hiyo kwa kumpata askofu mpya atakayechukua nafasi yake pasipo kuwepo kwa vurugu za aina yoyote tofauti na maeneo mengine ambayo pindi linapotokea zoezi la uchaguzi wa askofu huwa na vurugu kubwa .
Huku akisema kuwa hana ugomvi wowote na askofu wa Dayosisi Kusini Isaya Mengele kama ambavyo watu wanasema na kuwa mgogolo unaoendelea kati ya askofu huyo na waumini wake wa jimbo la Mufindi utatuzi wake ni maombi na sio kutumia nguvu. Alisema tayari amepokea maombi ya waumini wa jimbo la Mufindi kutaka kuhamia dayosisi ya Iringa na hana sababu ya kuwakataa kuwa pindi watakapokuwa tayari atawakaribisha.
Askofu Dr Mdegela aliyasema hayo leo wakati wa ibada maalum ya kumtambulisha Askofu mteule Mchungaji Blaston Gavile na msaidizi wake Himid Saga mbele ya waumini wa kanisa hilo Usharika wa Kanisa kuu, kuwa uchaguzi mkuu uliofanyika Ijumaa umemalizika kwa amani na utulivu mwingi na kupelekea heshima kubwa kwa dayosisi ya Iringa na Tanzania kwa ujumla.
" Tumemaliza uchaguzi wetu kwa amani na utulivu mwingi na hadi sasa hapa nimepokea salamu za pongezi kutoka Dayosisi mbali mbali na hata nje ya Tanzania wakipongeza kwa jambo hilo kufanyika pasipo kuwepo kwa vurugu zozote ....hii ni heshima kuwa imewekwa na yote haya yamewezekana kutokana na kazi nzuri ya waumini kufanya maombi "
Alisema kuwa hakuna jambo lolote alilolifanya vema pasipo kumtanguliza roho mtakatifu hivyo ombi lake kwa wale waliopewa kazi na Mungu ya kuongoza dayosisi hiyo ni kuepuka kusikiliza maneno ya watu wanayoyasema barabarani na badala yake kumtanguliza Mungu na kusikiliza kile kinachosemwa na viongozi wa dayosisi kwani maneno ya mitaani ni ya hivyo hivyo.
" Mimi yamesemwa mengi ila nawasamehe bure wale wote waliosema ila nawaomba baadae wote wakatubu wapo ambao walikuwa wakifanya kazi ya kunichafua katika vyombo vya habari na mitaani kwa kusema mambo ya aibu dhidi yangu ila kiuharisia sivyo hivyo ....kuna wengine ni maaskofu walipata kutamka kuwa mimi natumia vibaya fedha za chuo kikuu cha Iringa wakati wao ni wasomi na wanajua kabisa kuwa chuo kinakaguliwa na kuna taratibu nzuri tu za kifedha ila kwa kuwa walikuwa wanafanya hivyo kwa kufurahisha nafsi zao na kupotosha nasema ni wakati wa wote kutubu na wakitubu waje kuniomba msamaha "
Akifafanua juu ya ajenda ya waumini wa Kanisa hilo jimbo la Mufindi kutaka kuhama Dayosisi yao ya Kusini na kuhamia Dayosisi ya Iringa alisema kuwa kuwa ajenda hiyo ilizungumzwa na aliyewasilisha ajenda kwenye mkutano mkuu huo alikuwa ni yeye mwenyewe.
" wapo watu wanapotosha kuwa ajenda ya Mufindi kuhamia Dayosisi ya Iringa hakuzungumzwa kwenye mkutano mkuu nawaambia kuwa ajenda hiyo imezungumza na mimi ndie niliyeiwasilisha usiku wa octoba 6 mbele ya wajumbe kwa kutoa maelezo maana ajenda ya askofu ni ajenda ya mkutano mkuu hivyo sikuipeleka Halmashauri kuu wala kamati ya utendaji nilitoa taarifa kwenye mkutano huo kuwa Mufindi wameamua kuhamia Iringa tulipowauliza kuwa wanataka dayosisi walisema hapana wao wameamua kuhamia Dayosisi ya Iringa hivyo niliwaambia wajumbe kuwa hamuwezi ninyi kuwaambia wasihamie maana dayosisi ni mali ya Mungu si mali ya mwanadamu na wakihamia kuhamia popote wao wanaweza hivyo wajumbe wa mkutano huo walikubali kuwapokea ..... hoja ya pili wajumbe walisema kutokana na jambo hilo kuwa bado linasumbua kanisa waliniomba mimi Mdegela kuendelea kuliratibu jambo hilo hadi mwisho ila kuna uzushi umetokea kuwa katibu mkuu anasema ajenda hiyo haikuwepo ni kweli kabisa ajenda kubwa ilikuwa ni uchaguzi mkuu lakini ile nilisimama nikasema kama mimi kwa hiyo mimi nawajibika kusema mbele ya wajumbe na pia nawajibika kubaki na majibu ya ule mkutano mkuu yanayosema maamuzi ya waumini wa Mufindi ndio tutakaouheshimu ndio kauli ya mkutano mkuu "
Askofu Dkt Mdegela alisema kuwa watu wanasema kuwa msemaji wa dayosisi ya Iringa ni katibu mkuu wapo hao ni wapotoshaji na wanapaswa kupuuzwa kwani hadi sasa yeye Askofu ni msemaji mkuu wa dayosisi ya Iringa hadi hapo januari mwakani siku ambayo askofu mpya atasimikwa rasmi japo katibu mkuu anapaswa kusema kwa ruksa kutoka kwake hivyo anawataka waumini wa jimbo la Mafinga kupokea majibu ya maombi yao kuwa yamepokelewa rasmi.
Alisema kuwa waumini wa Mufindi waliomba kuhamia dayosisi ya Iringa baada ya kudai kuwa hawapendi kuendelea kubaki dayosisi ya kusini na hivyo walikuwa njia panda kwanza iwapo wangekataliwa Irinda walipanga kuanzisha kanisa lao ama kuanzisha dayosisi yao lakini si kubaki dayosisi ya Kusini.
" Mimi ni mtaalam wa Imani hivyo niliwajibu kwa barua kuwa cha kwanza kuwapatanisha na katibu mkuu na askofu wa dayosisi ya kusini pia kuombana msamaha pale walipokosana ......mimi sina chuki hata kidogo na askofu mwenzangu wa kusini Mengele amekuwa ni rafiki yangu siku zote walipokosana wakristo wa Mufindi na askofu wao Mengele ni pale walipokamatwa na kuwekwa mahabusu kijiji cha Mdandu na kunyimwa dhamana na kukosa kushiriki mkutano mkuu ambayo ni mamlaka kuu ya dayosisi na Halmashauri kubaki kimya juu ya suala hilo sasa mimi nasimamia ukweli kuwa mimi kama askofu sikutumwa kufunga watu polisi nimetumwa kuwakomboa wakristo ndio wanaochagua viongozi na wanayohaki ya kusikilizwa sio kufungwa gerezani sasa kama haya yanamkwaza mwenzangu sina jinsi huu ndio ukweli lakini tujiulize kama Yesu angewakuta pale mahabusu mdandu angefanya nini "
|
No comments:
Post a Comment