Friday, October 23

TAARIFA YA MKUU WA MKOA WA DODOMA CAPT CHIKU GALLAWA KUHUSU UCHAGUZI MKUU WA OKTOBA 25, 2015 MKOANI DODOMA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
Mkoa wa Dodoma
Anwani ya Simu REGCOM
Simu Nambari: 2324343/2324384
E-Mail No. ras@dodoma.go.tz
Fax No. +255 026 2320046
          
  Kateni Msitaafu Chiku Gallawa [RC]
    Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,
                            S.L.P.  914,
                              DODOMA.
Ndugu wananchi wa Mkoa wa Dodoma, tarehe 25 Oktoba, 2015 ni siku ya Uchaguzi Mkuu hapa nchini; ambapo, Watanzania wale wenye sifa za kupiga kura na waliojiandikisha, watapata fursa na kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi mbalimbali wa nchi yetu, kuanzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani.
Maandalizi ya kufanikisha zoezi la Uchaguzi Mkuu kwa Mkoa wa Dodoma yamekamilika. Hadi kufikia siku ya leo tayari wasimamizi wa uchaguzi wa wilaya zote saba za Mkoa wa Dodoma wameshapokea vifaa vyote vitakavyo tumika kwenye zoezi la uchaguzi. 
 
Hadi tunavyozungumza sasa, vifaa hivyo vinapelekwa kwenye vituo vya kupigia kura.
Vilevile, wasimamizi wa uchaguzi kwenye wilaya zote saba za Mkoa wa Dodoma wameshapokea fedha za kuendeshea uchaguzi Mkuu.  Aidha, Mafunzo kwa watendaji wote watakaoshiriki katika zoezi la uchaguzi yanahitimishwa kwenye wilaya za Dodoma.
 
Mkoa wa Dodoma tumefanikiwa kuandikisha jumla ya wananchi 1,053,136 kuwa wapiga kura sawa na asilimia 102.74 ya lengo, ambapo lengo ilikuwa kuandikisha watu/wapiga kura 1,025,084, Hivyo, natumia fursa hii kuwataka wale wote waliojiandikisha kupiga kura katika Mkoa wa Dodoma, kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Jumapili Oktoba 25. 
 
Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa kuanzia saa 1:00 asubuhi na zoezi la kuhesabu kura litaanza saa 10:00 jioni.  
Natumia fursa hii kusisitiza mambo machache ya muhimu kwenye zoezi la uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma na wadau mbalimbali wanaoshiriki Uchaguzi Mkuu kama ifuatavyo:
·        Wananchi wale wenye sifa za kupiga kura, wanahimizwa kwenda kupiga kura kwa amani na utulivu kwa kuzingatia muda na kisha kurejea makwao/majumbani baada ya kumaliza kupiga kura.
 
·        Viongozi wa vyama vya siasa na wagombea wa nafasi mbalimbali wawaandae wanachama na wafuasi wao kwenda kupiga kura, bila kuvunja sheria za uchaguzi, taratibu na kanuni zilizowekwa; wakidumisha hali ya Amani na utulivu.
 
·        Hairuhusiwi kwa mtu yeyote siku ya uchaguzi kufanya kampeni ya aina yoyote wala kuvaa mavazi ya chama chochote cha siasa.
 
·        Hairuhusiwi kwa mtu yoyote kutoa Rushwa kwa lengo la kumshawishi mtu kupiga kura au kumshawishi asipige kura.
 
·        Kila mtu aliyejiandikisha kupiga kura atunze shahada yake ya kupigia kura na asiitoe kwa mtu mwingine wala yeye kutumia shahada ya mtu mwingine kwani ni kosa la jinai kutumia shahada ya mtu mwingine kupigia kura. vilevile ni kosa kutumia shahada bandia.
 
·        Ni vizuri kila mmoja akahakikishe jina lake kwenye kituo alichojiandikishia ili kupata uhakika wa kuwepo kwenye orodha na kupiga kura kabla ya siku ya kupiga kura Oktoba 25.
 
·        Wananchi wote wakae katika hali ya utulivu wasiwe na hofu wala woga, Jeshi la polisi litafanya doria mbalimbali zenye lengo la kuhakikisha kunakuwa na hali ya Utulivu na hali ya Amani ili kila mtu apate fursa ya kushiriki zoezi la Uchaguzi.
Kabla sijahitimisha salamu zangu, narudia kuwasisitiza Wananchi wote wa Dodoma wale wenye sifa za kupiga kura wajitokeze kwa wingi kupiga kura siku ya Jumapili, Serikali imejiandaa vya kutosha na kuwahakikishia wananchi uchaguzi Mkuu kufanyika kwa amani, utulivu na kuwa uchaguzi wa Huru na Haki.
 
Nawaomba wananchi wote wajiepushe na vitendo vyovyote vinavyosababisha vurugu na Uvunjifu wa Amani; tuendeleze sifa yetu ya Mkoa wa Dodoma kufanya Uchaguzi tukiwa katika hali ya usalama.
Mwisho kabisa, nawatahadharisha wale wote wenye nia mbaya au wanaojipanga kutaka kujaribu kuvuruga zoezi la uchaguzi au kuleta vurugu ya aina yoyote hapa Mkoani Dodoma kuwa,  vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga imara na vitamshughulikia mara moja mtu huyo. Wananchi mnaombwa kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama au kwa kiongozi yoyote wa eneo husika.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
Imetolewa na:
OFISI YA MKUU WA MKOA WA DODOMA
Oktoba 23, 2015

BAADA YA MADAI YA UTOVU WA NIDHAMU HII NDIO KAULI YA DIEGO COSTA

Mshambuliaji wa klabu ya Chelsea Diego Costa ambaye amekuwa akiingia katika headlines kutokana na baadhi ya matukio yake anayoyafanya uwanjani, October 23 ameingia katika headlines tena baada ya kusema kuwa hawezi kubadilika kutokana na watu wanavyotaka na kufikiria.

Diego Costa amekuwa akiingia katika headlines kutokana na vitendo vyake vya utovu wa nidhamu, Diego Costa tayari alishafungiwa mechi tatu mwaka huu katika vipindi viwili tofauti tofauti. Costa alifungiwa mechi tatu kutokana na kugombana na beki wa Arsenal Laurent Koscielny na kumkanyaga kwa makusudi beki wa Liverpool Emre Can.

“Sitobadilika hivyo kwa sababu ya watu wanavyoweza kufikiria, baadhi ya watu wanaweza kufikiria mchezo wa mpira wa miguu ni kama ukumbi wa michezo kuwa kila mmoja anaweza kufanya vizuri. Lakini nafikiria mtu hubadilika pale unapovuka mstari mweupe wa kuingia uwanjani na unakuwa mtu tofauti na pale unapokuwa nje ya uwanja, ila ninapokuwa uwanjani naenda kupambana kwa ajili ya timu yangu na kuhakisha nafanya vizuri”>>> Diego Costa

MAHAKAMA: MARUFUKU MITA MIAMBILI, PIGA KURA, RUDI NYUMBANI

Mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam imetoa maamuzi ya kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na kada wa Chadema aliyekuwa akiiomba mahakama hiyo kutoa uamuzi wa kwamba wananchi wanatakiwa kukaa mita ngapi baada ya kupiga kura.


Mahakama hiyo imelitolea suala hilo ufafanuzi na kusema kuwa ni marufuku kwa wananchi kukusanyika katika kituo cha kupigia kura na hata njee ya mita 200 hairuhusiwi kwani ni kinyume cha sheria.


Kesi hiyo namba 37 ya mwaka huu, ilifunguliwa na mgombea ubunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chadema, Amy Kibatala, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) chini ya hati ya kiapo cha dharura.


Oktoba 16, mwaka huu, mlalamikaji alifungua kesi ya kikatiba iliyopewa usajili namba 37, ya mwaka huu akiiomba Mahakama itoe tafsiri ya kifungu cha 104 kidogo cha (1) cha Sheria ya Uchaguzi kama kinazuia ama kuwaruhusu wananchi kukaa kwa utulivu umbali wa mita 200, baada ya kupiga kura katika vituo.

Monday, October 19

AU YAUNDA JESHI LA PAMOJA AFRIKA



Kikosi kipya cha majeshi ya umoja wa Afrika kinafanya mazoeozi yake ya kwanza hii leo nchini Afrika Kusini.

Mazoezi hayo yanalenga kutathmini utayari wa kikosi hicho kutumika wakati kunapotokea dharura na kunahitajika kikosi cha mbele kitakachodhibiti hali na kuokoa maisha ya watu.

Lakini swali ibuka ni je jeshi hilo litatumwa katika taifa lililochangia wanajeshi wake ?

Mwandishi wa BBC anayeshughulikia maswala ya kiusalama Tomi Oladipo, anasema kuwa madhumuni ya kikosi hicho cha wanajeshi 25,000 kutoka mataifa ya bara Afrika ni kupunguza kutegemea kwa majeshi ya mataifa ya ulaya kuja humu barani kusuluhisha migogoro inayotokea.




Kikosi hicho kinatarajiwa kuanza oparesheni yake ya kwanza mwezi januari mwakani.

Hata hivyo umoja wa Afrika unasema unahitajika takriban dola bilioni moja kufadhili shughuli na oparesheni za kikosi hicho.

Mwandishi wa BBC anayeshughulikia maswala ya kiusalama anasema kuwa kuna changamoto za ukosefu wa ushirikiano mwema baina ya mataifa shirika.




Vilevile anasema kuwa mataifa mengi hayajajitolea kuunga mkono jeshi hilo kisiasa.
Jeshi hilo linatarajiwa kuwa na vikosi vitano.

Kwa sasa Cameroon imejitolea kuwa mwenyeji wa kikosi hicho ikisema watakita kambi yao katika mji wa Douala.

                                             bbcswahili.com