JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
Mkoa wa Dodoma
Anwani ya Simu REGCOM
Simu Nambari: 2324343/2324384
E-Mail No. ras@dodoma.go.tz
Fax No. +255 026 2320046
|
Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa,
S.L.P. 914,
DODOMA.
|
Maandalizi ya kufanikisha
zoezi la Uchaguzi Mkuu kwa Mkoa wa Dodoma yamekamilika. Hadi kufikia siku ya
leo tayari wasimamizi wa uchaguzi wa wilaya zote saba za Mkoa wa Dodoma
wameshapokea vifaa vyote vitakavyo tumika kwenye zoezi la uchaguzi.
Hadi
tunavyozungumza sasa, vifaa hivyo vinapelekwa kwenye vituo vya kupigia kura.
Vilevile, wasimamizi wa uchaguzi
kwenye wilaya zote saba za Mkoa wa Dodoma wameshapokea fedha za kuendeshea
uchaguzi Mkuu. Aidha, Mafunzo kwa
watendaji wote watakaoshiriki katika zoezi la uchaguzi yanahitimishwa kwenye
wilaya za Dodoma.
Mkoa wa Dodoma tumefanikiwa kuandikisha jumla ya
wananchi 1,053,136 kuwa wapiga kura
sawa na asilimia 102.74 ya lengo, ambapo
lengo ilikuwa kuandikisha watu/wapiga kura 1,025,084,
Hivyo, natumia fursa hii kuwataka wale wote waliojiandikisha kupiga kura katika
Mkoa wa Dodoma, kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Jumapili Oktoba 25.
Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa kuanzia saa 1:00 asubuhi na zoezi la kuhesabu kura litaanza saa 10:00 jioni.
Natumia fursa hii kusisitiza mambo machache ya muhimu
kwenye zoezi la uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma na
wadau mbalimbali wanaoshiriki Uchaguzi Mkuu kama ifuatavyo:
·
Wananchi wale wenye
sifa za kupiga kura, wanahimizwa kwenda kupiga kura kwa amani na utulivu kwa
kuzingatia muda na kisha kurejea makwao/majumbani baada ya kumaliza kupiga
kura.
·
Viongozi wa vyama
vya siasa na wagombea wa nafasi mbalimbali wawaandae wanachama na wafuasi wao
kwenda kupiga kura, bila kuvunja sheria za uchaguzi, taratibu na kanuni
zilizowekwa; wakidumisha hali ya Amani na utulivu.
·
Hairuhusiwi kwa mtu
yeyote siku ya uchaguzi kufanya kampeni ya aina yoyote wala kuvaa mavazi ya
chama chochote cha siasa.
·
Hairuhusiwi kwa mtu
yoyote kutoa Rushwa kwa lengo la kumshawishi mtu kupiga kura au kumshawishi
asipige kura.
·
Kila mtu
aliyejiandikisha kupiga kura atunze shahada yake ya kupigia kura na asiitoe kwa
mtu mwingine wala yeye kutumia shahada ya mtu mwingine kwani ni kosa la jinai
kutumia shahada ya mtu mwingine kupigia kura. vilevile ni kosa kutumia shahada
bandia.
·
Ni vizuri kila mmoja
akahakikishe jina lake kwenye kituo alichojiandikishia ili kupata uhakika wa kuwepo
kwenye orodha na kupiga kura kabla ya siku ya kupiga kura Oktoba 25.
·
Wananchi wote wakae
katika hali ya utulivu wasiwe na hofu wala woga, Jeshi la polisi litafanya
doria mbalimbali zenye lengo la kuhakikisha kunakuwa na hali ya Utulivu na hali
ya Amani ili kila mtu apate fursa ya kushiriki zoezi la Uchaguzi.
Kabla sijahitimisha salamu zangu, narudia
kuwasisitiza Wananchi wote wa Dodoma wale wenye sifa za kupiga kura wajitokeze
kwa wingi kupiga kura siku ya Jumapili, Serikali imejiandaa vya kutosha na
kuwahakikishia wananchi uchaguzi Mkuu kufanyika kwa amani, utulivu na kuwa
uchaguzi wa Huru na Haki.
Nawaomba wananchi wote wajiepushe na vitendo
vyovyote vinavyosababisha vurugu na Uvunjifu wa Amani; tuendeleze sifa yetu ya
Mkoa wa Dodoma kufanya Uchaguzi tukiwa katika hali ya usalama.
Mwisho kabisa, nawatahadharisha wale wote wenye
nia mbaya au wanaojipanga kutaka kujaribu kuvuruga zoezi la uchaguzi au kuleta
vurugu ya aina yoyote hapa Mkoani Dodoma kuwa,
vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga imara na vitamshughulikia mara
moja mtu huyo. Wananchi mnaombwa kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama
au kwa kiongozi yoyote wa eneo husika.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
Imetolewa na:
OFISI
YA MKUU WA MKOA WA DODOMA
Oktoba 23, 2015
No comments:
Post a Comment