Wednesday, April 13

KAMANDA WA POLIS MWANZA AWATAKA POLIS KUWAKABILI MAJAMBAZI KWA NGUVU ZOTE....


Kamanda mpya wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Ahmed Msangi amewataka polisi kukabiliana na majambazi kwa nguvu zote na ikibidi kuwaua kabla hawajasababisha madhara makubwa kwa raia.

Msangi ambaye amehamia mkoani Mwanza  akitokea  jijini Mbeya, ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na maofisa usalama na polisi wa vyeo mbalimbali baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi hiyo na SACP, Justus Kamugisha.

Msangi ametoa kauli hio siku chache baada ya John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kusema kwamba, Kamugisha alikuwa mzigo kwenye jiji hilo kutokana na kushindwa kukabiliana na ujambazi.

Katika kipindi cha miezi miwili ya Machi na Aprili mwaka huu, matukio saba ya uhalifu wa kutumia silaha za moto yameripotiwa na katika matukio hayo watu sita walipoteza maisha.

Msangi amesema kuwa, anawashangaa polisi wanaoshindwa kutumia silaha zao kuwakabili watu wanaodaiwa kuwa majambazi na kusababisha vitendo vya uhalifu kuendelea kushamiri jijini humo.

“Tumieni na nyie bunduki zenu kuyaua majambazi. Mbona wao wanaua raia? Haiwezekana uwe na silaha halafu unaacha kuchukua hatua za haraka za watu ambao wanasababisha mauaji na uporaji wa mali za raia,” amesema Msangi.

Msangi amesema, Jiji la Mwanza miezi michache iliyopita limetikiswa na matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha yanayoambatana na mauaji ya raia, kujeruhi na uporaji wa mali zao.

Amesema kuwa, polisi wanapaswa kufanya kazi zao kwa kujiamini na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Kamanda Kamugisha akikabidhi ofisi hiyo aliwahimiza polisi kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia maadili ya jeshi hilo bila kumuonea mtu yeyote yule.

No comments: