Wednesday, March 2

Wahukumiwa miaka 120 na kulipa fidia ya Bilioni 1.4

 

6a00d83455b3db69e201347fedbbb7970c
Mahakama ya hakimu mkazi Singida imewahukumu washitakiwa sita adhabu ya kutumikia jela jumla ya miaka 120 na kulipa faini ya jumla ya zaidi ya shilingi Bilioni 1.4, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumiliki kinyume na sheria vipande 53 vya tembo vyenye thamani ya shilingi 149,336,000 na kosa la jingine la uwindaji.


Washitakiwa hao ni Eliud Selema Mayunga (38) mkazi na mkulima wa kijiji cha Kiombo,Ramadhani Said Biladuka (47) mkulima mkazi wa Itigi,Lenard Oscar Sunzu (31) mkazi wa kijiji cha Karangari,Pilimon Michael Kanyonga (31) mkazi wa Kitaraka Itigi,Iddi Waziri Issah Ustadh (30) mkazi wa kijiji cha Kiombo na Jimmy Charles Lyimo (39) mfanyabiashara wa Tabora Kyombo.


Mwendesha mashitaka na mwanasheria wa serikali Petrida Mutta alidai mbele ya hakimu mfawidhi mwandamizi wa mahakama hiyo, Jocye Minde kuwa mnamo Machi, 31 mwaka 2014, muda usiojulikana washitakiwa kwa pamoja walikamatwa wakiwa wamehifadhi na kumiki vipande hivyo 53 vya meno ya tembo nyumbani kwa mshitakiwa Issa Ustadh, huku wakijua wazi kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria.


Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo mwanasheria wa serikali, Mutta aliiomba mahakama hiyo kuwapa washitakiwa adhabu kali ili iwe fundisho kwao.


“Mheshimiwa kwa sasa tunaendelea kusikia na kuona vitendo vya uwindaji na biashara za nyara za serikali vikiendelea kushamiri, vitendo hivi haviwezi kufumbiwa macho kwa sababu vikifumbiwa macho, fahari ya nchi hii ya wanyama pori itatoweka naiomba mahakama yako itoe adhabu kali si tu iwe fundisho kwa washitakiwa mbali iweze kuwaonya na watu wengine wanaotaka kujihusisha na uwindaji na biashara haramu ya nyara za serikali,” alisema mwanasheria huyo wa serikali.


Kwa upande wa washitakiwa ambao wakili wao Mr. Josephat Raphael Wawa hakuwepo wakati hukumu hiyo inatolewa kila mmoja kwa nafasi yake aliiomba mahakama hiyo impe adhabu nafuu.


Akitoa hukumu hiyo iliyosikilizwa na umati mkubwa wa wananchi, hakimu Minde alisema upande wa jamhuri imethibitisha bila kuacha shaka yoyote kwamba washitakiwa wanayo hatia kwa makosa yote mawili.


“Kwa kosa la kwanza la kumiliki kinyume na sheria vipande 53 vya meno ya tembo,kila mmoja wenu atatumikia jela miaka 20 na kila mmoja wenu, atalipa faini ya shilingi 248,893,333.30 kwa kosa la pili la kujihusisha na uwindaji haramu,kila mmoja wenu,” alisema hakimu.



No comments: