Thursday, March 10

KUBENEA AKAMATWA NA JESHI LA POLIS AJUMUISHWA KESI YA UCHAGUZI WA MEYA DAR


MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea amekamatwa na Jeshi la Polisi leo asubuhi wakati akiwa katika Mahakama ya Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Kubenea amekamatwa na polisi akituhumiwa kushiriki kumpiga Terresia Mmbando, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Mmbando alikuwa mwenyekiti wa mkutano wa kumchagua Meya wa Jiji la Dar es Salaam uliofanyika wiki mbili zilizopita na baadaye kuahirishwa hatua ambayo iliibua malumbano.

Kubenea  alikwenda leo mahakamani kuendelea na kesi yake inayohusu kumtukana Paul Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.

Kesi hiyo ilifunguliwa tarehe 15 Desemba mwaka jana baada ya wawili hao kukutana kwenye Kiwanda cha Nguo cha TOOKU kilichopo Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Katika tuhuma za kumpiga Mmbando, waliokamatwa katika hatua ya kwanza ni Halima Mdee, Mbunge wa Kawe; Mwita Waitara, Mbunge wa Ukonga na madiwani wawili ambao kwa sasa wapo nje kwa dhamana.

Baada ya kupata dhamana Mdee alisema “Watake wasitake wataachia, hapa ni Ukawa tu. Yote haya yana mwisho lakini wajue kuwa namba ‘zinatufeva’ na si vinginevyo.”

Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar s Salaam ndio chanzo cha kukamatwa kwa Kubenea na wengine waliotangulia ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimekuwa vikisigana.

Ukawa wanalalamika kuminywa na Halmashauri ya Jiji kwa madai ya kushirikiana na CCM. Ukawa wameeleza kuwa zinafanyika hujuma ili CCM ishinde Umeya wa Jiji.

Jumla ya wajumbe wa mkutano wa kumchagua Meya wa Jiji ni 161. Kwa upande wa Kinondoni kuna wajumbe 58 ambapo CCM wapo 20 na ukawa 38.

Temeke jumla ya wajumbe 49, CCM wapo 31 na ukawa 18 na Ilala jumla ya wajumbe 54 huku CCM wakiwa 23 ukawa 31.

No comments: