Serikali ya
Marekani imeshauri Raia wake walio nchini Burundi kuondoka nchini humo
haraka iwezekanavyo baada ya watu 87 kuuawa kwenye ghasia zilizotokea
siku ya Ijumaa.
Ghasia zilizojitokeza kwenye mitaa ya mji mkuu wa
nchi hiyo, Bujumbura ni mbaya zaidi tangu kuanza kwa vurugu mwezi Aprili
baada ya Rais Pierre Nkurunziza kuamua kuwania tena urais kwa muhula wa
tatu.Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Human Rights Watch (HRW) limeitisha uchunguzi kuhusu mauaji hayo ya Ijumaa.
Mwezi uliopita, Ubelgiji pia iliwashauri raia wake kuondoka Burundi, huku Muungano wa Ulaya (EU) nao ukipunguza wahudumu wake, kwa kuondoa wafanyakazi ambao ni wa muda, "familia na wafanyakazi ambao si muhimu sana."
"Kufuatia machafuko ambayo yanaendelea kuongezeka, Wizara ya Kigeni meagiza kuondoka kwa jamaa za maafisa wa Marekani na maafisa ambao si wa kushughulikia dharura nchini Burundi," taarifa ya Marekani ilisema.
"Ubalozi wa Marekani unaweza kutoa huduma za dharura kwa kiwango cha chini tu kwa raia wake nchini Burundi."
Jijini Nairobi, wanaharakati Jumapili jioni waliwakusanya vijana kutoka Burundi, Kenya na nchi nyingine za Afrika Mashariki jijini Nairobi kwa ajili ya mkesha na kuwasha mishumaa kuwakumbuka Raia wa Burundi walioathirika kutokana na mzozo wa kisiasa nchini mwao.
Aidha, walitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuingilia kati.
No comments:
Post a Comment