Monday, December 14

Zuma amteua waziri mwingine wa fedha...


Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amemteua waziri mwingine wa fedha katika kipindi cha siku nne, baada ya uteuzi wa awali kupingwa vikali.
Bw Zuma alikuwa amemfuta kazi Nhlanhla Nene wiki iliyopita na kumteua Desmond Van Rooyen kuwa waziri mpya.
Hatua hiyo ilipingwa vikali na watu huku masoko yakidorora na thamani ya sarafu ya Rand ikishuka pakubwa.
Uteuzi huo pia ulishutumiwa kupitia mitandao ya kijamii, kitambulisha mada #Zumamustfall kikivuma sana Afrika Kusini.
Kutokana na hayo, Rais Zuma ameamua kubadilisha uamuzi wake na kumteua Pravin Gordon ambaye amewahi kuwa waziri wa fedha.
Bw Gordon ndiye aliyemtangulia Bw Nene katika Hazina Kuu na alisaidia kuongoza taifa hilo kupitia msukosuko wa kudorora kwa uchumi 2009.
Mwandishi wa BBC aliyeko Johannesburg Matthew Davies anasema sarafu ya Rand ilianza kuimarika Jumapili na bei ya hisa katika Soko la Hisa la Johannesburg inatarajiwa kuanza kupanda tena wiki hii.
Hata hivyo, hali ya Bw Zuma kuonekana kutokuwa na msimamo itaathiri sana chama tawala cha ANC huku taifa hilo likijiandaa kwa uchaguz wa serikali za mitaa mwaka ujao.

No comments: