Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema leo kimefungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, ili kuiomba Mahakama hiyo kutengua zuio la kuuaga mwili wa aliekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Geita Marehemu Alphonce Mawazo, lililotolewa na Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza kutokana na hofu ya kiusalama pamoja na uwepo wa ugonjwa wa Kipindupindu.
Katika kesi hiyo, Chadema inawakilishwa na Mawakili watatu ambao ni James Millya, John Mallya pamoja na Paul Kipeja ambapo mlalamikaji ni Charles Lugiko ambae ni baba mdogo wa Marehemu Mawazo.
Mahamaka hiyo chini ya Jaji Lameck Mlacha, imesikiliza malalamiko ya upande wa washtaki na kuahirisha kesi hiyo hadi kesho ambapo imeamuru mlalamikiwa ambae ni Mkuu wa Polisi Mkoa wa Mwanza pamoja na mwanasheria Mkuu wa Serikali kupelekewa nyaraka za kesi hiyo kabla ya kusikiliza utetezi wao hapo kesho.
Mapema kabla ya kesi hiyo kusikilizwa, wafuasi wa Chadema waliokuwa wamekusanyika nje ya viunga vya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, walilalamikia hatua ya jeshi la polisi kuwazuia kuingia Mahakamani hapo ili kujua hatima ya kesi hiyo, ambapo wamesema kitendo hicho kinaondoa dhana ya Rais John Pombe Magufuli, kuwa yeye ni rais wa wananchi wote wakati wao kama Chadema wananyimwa haki zao.
Licha ya Malalamiko hayo pamoja na ulinzi mkali wa polisi uliokuwa umetanda Mahakamani hapo, bado wafuasi wa Chadema hawakuondoka katika viunga vya Mahakama hiyo hadi pale Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Freeman Mbowe alipowasihi kurejea majumbani mwao hadi kesho kesi hiyo itakaposikilizwa tena.
Ni zaidi ya siku nane sasa tangu marehemu Alphonce Mawazo auawe kikatili Mkoani Geita na watu wasiojulikana kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni chuki za kisiasa ambapo mwili wake umehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando.
No comments:
Post a Comment