Wednesday, September 23

HABARI KUTOKA RASI FM RADIO..SEPT 23 MCHANA



picha na Maabara
DODOMA                     

Waumini wa dini ya kiislamu duniani kote wanatarajia kusherehekea sikukuu ya Eid El Hajj hapo kesho ambapo kwa mkoa wa Dodoma ibada ya pamoja  ya sikukuu ya swala ya eid el hajj I itakuwa katika uwanja wa jamhuri.


Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari naibu katibu mkuu wa kamati za sherehe za kiislamu wa Dodoma mjini Rajab Hussein imewataka waumini wa mjini Dodoma na viunga vyake kufika maeneo hayo mapema kwa ajili ya kufanya ibada na sherehe hiyo itakayoanza saa moja kamili.

Pamoja na waumini wa kiislamu pia taarifa hiyo imeeleza kuwa waumini wa dini nyingine wanaruhusiwa kuhudhuria ibada hiyo kwani wao nao wanaweza kushiriki katika ibada na sherehe za Eid El Hajj ili washuhudie kheri na kupokea dua, ambapo kisheria ibada hiyo huswaliwa sehemu ya wazi isipokuwa kwa dharura ndio yaweza kufanyikia msikitini.

Ibada hiyo ya pamoja ya sikukuu ya Eid El Hajj mwaka huu wa 2015 ambao ni sawa na mwaka 1436 kwa mwaka wa kiislamu ni kuhuwisha Sunna ya mtume Nabii Muhammad {S.A.W}ambapo inategemea mwandamo wa mwezi kumi Dhul Hijja.

Na Denis kazenzele Dodoma                                                                                          

______________________________________________________________________________
 DAR ES SALAAM             
   
Taasisi ya Sekta binafsi nchini imewakaribisha wawekezaji kutoka Marekani kuja nchini kuwekeza kwa ubia na Watanzania kwa vile Tanzania kuna amani na imejaliwa utajiri mkubwa wa raslimali za asili zinazohitaji kuendelezwa.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania – TPSF Dr Reginald Mengi ametoa rai hiyo jijini Dar es salaam wakati Ujumbe wa TPSF ulipokutana na ujumbe wa serikali ya jimbo la Alabama la nchini Marekani, ulioongozwa na Waziri wa Biashara wa jimbo hilo Bw. Gred Canfield.
  
Kwa upande wake Waziri wa Biashara wa Jimbo la Alabama Bw. Greg Canfield amesema ujumbe wake upo nchini kutafuta fursa za uwekezaji kwa ajili ya wafanyabiashara wake, na kusisitiza kuwa mazingira mazuri ya kisiasa, urahisi wa kuwekeza, na uwepo wa miundombinu ya msingi ni miongoni mwa mambo yatakayowavutia wawekezaji wa Alabama kuwekeza kwa ubia hapa nchini.

Akiutoa mashaka ujumbe huo kuhusu mazingira ya uwekezaji nchini,Mkurugenzi Mkuu wa TPSF Bw. Godfrey Simbeye amesema serikali ya Tanzania imechukua hatua madhubuti kuboresha mazingira ya uwekezaji, na kusisitiza kuwa msisitizo huo upo pia katika katiba mpya ijayo.

Wakati wa mkutano huo, uliowashirikisha wadau mbalimbali wa taasisi ya sekta binafsi, na baadhi ya viongozi wa taasisi za serikali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa bodi ya Utalii Tanzania Bi. Devota Mdachi ameuelezea ujumbe huo kuhusu vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo hapa nchini.


Na Denis kazenzele Dodoma   

______________________________________________________________________________
MWANZA                             

Zaidi ya wanachama 500 wa Chama cha Walimu Tanzania CWT wilayani Nyamagana wameandamana hadi katika ofisi za mkurugenzi wa jiji la Mwanza wakihitaji kupewa majibu sahihi juu ya madai yao ya mishahara, malipo ya likizo, nauli, posho, matibabu pamoja na kupandishwa vyeo.

Kwa mujibu wa walimu hao, madai hayo ni ya muda mrefu, licha ya kupaza sauti zao kupitia Chama cha Walimu nchini CWT lakini hawakupatiwa majibu sahihi juu ya madai hayo.

Hata hivyo Mkurugenzi wa jiji la Mwanza amekutana  na waandishi wa habari na kueleza  kushangazwa na hatua hiyo kwa madai kuwa jiji halina mgogoro na walimu wala watendaji wa sekta yoyote.

Madeni ambayo walimu wanadai kutolipwa tangu mwaka 2008 ni zaidi ya shilingi milioni 600 hatua ambayo inapingana na taarifa ya mkurugezi inayodai walimu hao wanadai shilingi milioni mia moja na saba laki tatu 54 elfu na sitini pekee.

Licha ya walimu hao kuombwa kurejea ukumbini ili kukutana na mkurugenzi kuendelea na kikao, jitihada hizo hazikuzaa matunda kwani walihitaji waandishi wa habari nao washiriki kikao hicho ambacho viongozi wa jiji walidai ni kikao cha ndani hivyo kwa mujibu wa taratibu za kiutumishi hakikuhitaji wanahabari.

Hatua hiyo imesababisha kuvunjika kwa kikao hicho ikidaiwa kuwa watapanga siku mbadala ya kukutana na kiongozi huyo.

Na Denis kazenzele Dodoma 

________________________________________________________________________________
DAR ES SALAAM                 

Imeelezwa kuwa jamii kubwa inayofanya shughuli za kiuchumi kwenye maeneo ya bandari iko kwenye hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa UKIMWI kutokana na kutokuwepo kwa mtandao unaotoa elimu ya kupambana na ugonjwa huo kwenye mazingira yao.

Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa utafiti ulioendeshwa na Taasisi ya Kimataifa inayojihusisha na kufuatilia usafirishaji haramu wa binadamu IOM kwa ushirikiano na Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC.

Taarifa hiyo inasema, elimu juu ya matumizi ya kinga bado ni changamoto kwa jamii hiyo hivyo wengi hujihusisha na ngono zisizo salama hatua inayotishia ongezeko la maambukizi mapya ya VVU.

Kwa mujibu wa Ripoti hiyo iliyozinduliwa Jijini Dar es Salaam inahusisha pia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UkIMWI (TACAIDS), inaonyesha baadhi ya watu wanaojishughulisha kwenye maeneo hayo, huanzisha uhusiano wa muda mfupi na watu tofauti, kutokana na asili ya kazi zao za kuhamahama.

Dk. Jerome Kamwela Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini TACAIDS amesema ripoti inawagusa zaidi watu wanao hamahama  pamoja na madereva wanaoendesha magari makubwa ya mizigo, ambayo kwa ujumla wake imekuwa ikiendekeza tabia hatarishi na kusababisha kuwa kwenye hatari kubwa zaidi.

Mwakilishi wa IOM Ukanda wa Kusini mwa Afrika, Dr. Erick Ventura amesema shughuli kama hizi za kiuchumi zenye asili ya kuhamahama zimekuwa zikikabiliwa na changamoto kubwa, hivyo kuzitaka mamlaka husika kupitia upya sera na programu za afya zinazogusa maeneo hayo.

Na Denis kazenzele Dodoma 
 ______________________________________________________________________________

KIMATAIFA

WASHINGTON                         

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewasili nchini Marekani kuanza ziara ambamo pia atahudhuria kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, na kuzungumza katika kikao cha Congress ya Marekani, ambacho kinajumuisha Baraza la Wawakilishi na Baraza la Seneti. 

Papa Francis mwenye umri wa miaka 78 alipokelewa na Rais wa Marekani Barack Obama na mkewe Michelle Obama katika uwanja wa ndege za kijeshi wa Andrews karibu na Washington DC. 

Makamu wa Rais Joe Biden pia alikuwepo kumpokea Papa Francis, ambaye alisafiri kutoka Cuba katika ndege ya kampuni ya Alitalia. 

Katika ziara yake ya siku tatu nchini Cuba, Papa Francis aliwataka raia wa nchi hiyo kuyazingatia mapinduzi mapya ya upendo na huruma na kujenga daraja pamoja na kupandikiza mbegu za maridhiano, wakati ambapo juhudi zinaendelea kurejesha uhusiano kati ya nchi hiyo na Marekani.


                                                            
Na Denis kazenzele Dodoma 

____________________________________________________________________________

OUAGADOUGOU            
Katika Kasri la Mogho Naba, Mfalme wa jamii ya Mossi (katikati akivaa nguo za kiraia), wanajeshi wa vikosi vya jeshi vinavyounga mkono serikali ya mopito na afisa wa kikosi cha ulinzi wa Rais (RSP) wakisaini makubaliano ya kutohasimiana Jumanne Septemba 22Kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi ya wiki iliyopita nchini Burkina Faso Jenerali Gilbert Diendere hii leo anatarajiwa kukabidhi madaraka kwa rais aliyempindua, Michel Kafando baada ya shinikizo kubwa kutoka viongozi wa kikanda. 


Makubaliano yamepatikana kati ya jenerali huyo na jeshi la nchi yake usiku wa kuamkia leo, hii ikiwa ni kwa mujibu wa wawakilishi wa pande hizo mbili. 

Makubaliano hayo yamejengwa juu ya vipengele vitano, ambavyo vinajumuisha kile kinachowataka wanajeshi wa kikosi cha ulinzi wa rais kilichojaribu kufanya mapinduzi - RSP, kurejea katika kambi yao, na kuondoka katika vituo walivyovikamata katika mji mkuu wa nchi hiyo, Ouagadougou. 

Jeshi nalo kwa upande wake limekubali kurudi nyuma umbali wa Km 50, na kuhakikisha usalama wa wanajeshi wa RSP pamoja na wa familia zao. 

Marais wa ECOWAS wanatarajiwa kusimamia shughuli ya kumrejesha madarakani Michel Kavando leo Jumatano.

Na Denis kazenzele Dodoma 
________________________________________________________________________________

ADEN                          
Baada ya miezi sita ya uhamishoni nchini Saudi Arabia, Rais wa Yemen Abd Rabbo Mansour Hadi amerejea katika mji wa Aden, mji mkuu wa kusini, uliyotangazwa mji mkuu wa "muda", ambapo kunapangwa mashambulizi kwa minajili ya udhibiti wa eneo la kaskazini mwa nchi linaloshikiliwa hadi sasa na waasi wa Kishia.
Hadi alikimbilia katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, baada ya kulazimishwa kuondoka mji wa Aden Machi 25, ambako alikimbilia kutokana na kusonga mbele kwa waasi wa Kishia wa Huthi, ambao wameendelea kuudhibiti mji mkuu Sana’a na sehemu kubwa ya nchi ya Yemen.

Hadi meahidi Jumanne usiku kurudi haraka katika mji wa Sanaa baada ya ukombozi wa miji yote na majimbo yanayoshikiliwa na wanamgambo waliofanya mapinduzi .

Kurudi kwake, siku mbili kabla ya Eid al-Adha, Sikukuu ya Kiislam, kunafuatia kurudi kwa Makamu Rais Khaled Bahah na mawaziri kadhaa wiki iliyopita katika mji wa Aden uliyodhibitiwa kutoka mikononi mwa waasi wa Kishia wa Huthi mwezi Julai mwaka huu.

Machafuko nchini Yemen yamesababisha vifo vya watu 4,900 na wengine 25,000 wamejeruhiwa tangu mwezi Machi, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Na Denis kazenzele Dodoma 



>>>>>>MWISHO<<<<<<

No comments: