Tuesday, September 22

RASI FM HABARI SAA 7:00 USIKU SEPT 22



Bukola SarakiDAR  ES  SALAAM                

Chama cha Wazazi wa Watoto Wenye Ulemavu wa Mtindio wa Ubongo, Akili na Viungo (Chawaumavita) kimewataka wakina baba kuacha tabia ya uoga ya kukimbia majukumu pindi wanapopata watoto wenye ulemavu.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Watu na Watoto Wenye Mtindio wa Ubongo ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo Oktoba 7, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Hilal Saidi, amesema watoto wenye matatizo hayo wanapaswa kusaidiwa badala ya kuwatenga.

Katika hatua nyingine chama hicho kimewaomba wagombea wa vyama mbalimbali vya siasa kuzungumzia namna gani watasaidia walemavu katika mikutano yao.

Amesema kuwa  katika tafiti walizofanya wamegundua kuwa wanaume wengi ni waoga wa majukumu pindi wanapopata watoto wenye ulemavu hadi kupelekea kukimbia famia zao.

Hata hivyo amesema ulemavu umegawanyika katika makundi matatu ambayo ni  ni ulemavu wa akili,mtindio wa ubongo na viungo.


Na John Banda/Denice/Josephine .....................................

_______________________________________________________________________

DODOMA                     

Mgombea udiwani kata ya Chitemo wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma kupitia chama cha mapinduzi [CCM] Donard Jeremia amesema kama wakazi wa kata hiyo watampa Ridhaa ya kuwa diwani wa kata hiyo atahakikisha anatatua kero za ukosefu wa Mawasiliano, Maji na Afya.

Mgombea huyo ameyasema hayo wakati akiwahutubia wakazi wa kijiji cha Chitemo wilayani humo alipokuwa kwenye mfululizo wa kampeni zake za kuomba kura.

Amesema baada ya kuchaguliwa ataanza na kuchimba visima virefu na vifupi katika vijiji vya Chitemo, Chibwejele, Mkanana na Ngalamilo ili wananchi wa vijiji hivyo waweze kupata maji safi na salama.

Mgombea huyo amesema kero hiyo ya ukosefu wa maji iliyopo katika kata yake inatokana na Miundo mbinu kuwa ya kizamani kwa sababu iliwekwa tangu mwaka 1970 hivyo ipo katika hali ya uchakavu.

Aidha amesema atahakikisha utunzaji wa mazingira unazingatiwa kwa wananchi kupanda miti ikiwa na kuwazuia wasikate miti wala kuchoma hovyo misitu.

Na John Banda/Josephine..............................................                                              
 _____________________________________________________________


 DAR  ES  SALAAM                   

Serikali ya Norway imesema itaendelea kuwa mdau mkuu wa maendeleo nchini Tanzania, hasa katika uimarishaji wa kilimo ili kutokomeza umasikini. 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Norway, Monica Maeland wakati wa uzinduzi wa kituo kikubwa cha mbolea cha Yara jijini Dar es Salaam uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete. 

Amesema kituo hicho hicho kitasaidia kukuza sekta ya kilimo na kukifanya kuwa chenye ushindani kwa wawekezaji wa kimataifa. 

Aidha Kilimo ni sekta inayoajiri zaidi ya asilimia 70 ya nguvu kazi ya taifa ambapo inachangia asilimia 25 katika pato la taifa (GDP), asilimia 34 ya fedha za kigeni na asilimia 125 ya mahitaji ya chakula. 

Akizindua kituo hicho, Rais Jakaya Kikwete amesema Yara imekuja kwa muda muafaka kwa kuwa mojawapo ya rasilimali zilizokuwa zikiumiza kichwa ni uigizaji mbolea na kuipata kwa wakati. 

Ameongeza kuwa mbali na tani 50,000 zinazozalishwa katika kiwanda cha Minjingu wilayani Babati katika mwaka 2015 uagizaji wa mbolea umeongezeka na kufikia tani 270,000. 

Hata hivyo Matumizi ya mbolea kwenye kilimo yamekuwa yakiongezeka kutoka tani 100,000 kabla ya mwaka 2010 hadi kufikia tani 200,000 mwaka huu.

Na Josephine .............................................

____________________________________________________________

IRINGA        
       
Wakati kampeni zikizidi kupamba moto Chama cha Mapinduzi CCM mkoa wa Iringa kimelalamikia matukio ya uvunjifu wa amani ambayo yamejitokeza katika mikutano ya kampeni Kuelekea Uchaguzi mkuu octoba 25 mwaka huu.

Chama hicho kimesema matukio hayo kwa kiwango kikubwa yameendeshwa na baadhi ya vijana ambao wanatumiwa kuvuruga amani jambo ambalo halipaswi kuvumiliwa,hivyo kimewataka viongozi wa kisiasa kuendesha siasa za kistaarabu zenye dira ya demokrasia itakayotunza tunu za Taifa.
Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa Bwana Hassan Mtenga amewataka vijana kutumia busara kwa kuwapuuza viongozi wenye nia ya kuvuruga amani Kwenye mkutano wa hadhara wa chama cha mapinduzi CCM katika Kata ya Kihesa mjini Iringa. 
Aidha Mtenga amesema kiongozi yoyote anayehamasisha matukio ya uvunjifu wa amani, hafai kamwe kuwa kiongozi, huku akiwaasa wananchi kuacha ushabiki katika jambo muhimu la kuwapata viongozi.

Pamoja na hayo pia Amewasihi vijana na wananchi kwa ujumla kutokihukumu Chama cha mapinduzi na badala yake watoe ushauri wa nini kifanyike ili kukiboresha chama hicho.

Na Josephine ................................................  

___________________________________________________________________________


 DAR  ES  SALAAM             
 
Serikali imeahidi kumaliza mgogoro uliopo kati ya mmiliki wa eneo la Magereji Wazohill na wamiliki wa gereji zilizopo katika eneo hilo baada ya kujiridhisha kwa mipaka yake.

Imeelezwa kuwa Mgogoro wa eneo hilo umedumu kwa muda mrefu bila utatuzi wowote kutoka kwa Serikali ambayo iliwakabidhi wananchi kufanya shughuli zao katika eneo hilo.
Wafanyabiashara wa eneo hilo la Magereji walikabidhiwa na Manispaa ya Kinondoni 2005 baada ya kuvunjwa kwa gereji bubu na kutengewa eneo maalumu na baadaye Mwenge wa Uhuru kuweka jiwe la msingi.
Akiwahakikishia wananchi wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi, Angela Kairuki amesema Serikali inalitambua hilo na inalifanyia kazi ili haki itendeke ili kila mmoja aweze kufanya shughuli zake kwa uhuru zaidi.
Aidha amewataka wafanyabiashara waliowekeza shughuli zao katika eneo hilo kuwa na uvumilivu na kufuata taratibu na sheria za nchi zilizowekwa wakati Serikali ikifanya mchakato wa kupima upya eneo hilo.

na Josephine Charles....................................      

KIMATAIFA


 KAMPALA                    
 

Serikali ya Uganda inatafuta kubuni mbinu mpya ya kunufaika na soko la bidhaa la Marekani. 

Wataalamu wa uchumi wa nchi hiyo wamesema Uganda inahitaji ujuzi na maarifa ya kuvuna pakubwa kwenye soko la ukuwaji wa Afrika na Marekani AGOA. 

Uganda inalenga kutumia sekta za nguo,matunda,kahawa ,madini na petroli kuongeza mapato ya jumla ya nchi hiyo. 

Mwenyekiti wa mipango maalum ya kitaifa ya Uganda Kisamba Mugerwa amesema wanahitaji soko bora la bei imara. 

Aidha Vikao maalum vya majadiliano ya biashara na uwekezaji vitaanzishwa katika kila mkoa.

Josephine Charles............................      
____________________________________________________________


 DAMASCUS    
                  
Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya jeshi la serikali ya Syria na jeshi la upinzani, pande hizo mbili zimeanza kusimamisha mapigano katika sehemu tatu, na baadaye zitasimamisha mapigano kwa muda wa miezi sita. 

Kutokana na makubaliano hayo, vikosi vya upinzani vitaondoka kutoka Zabadani. Wakati huohuo, majeruhi, wanawake, watoto na wanaume wenye umri zaidi ya miaka 50 wataruhusiwa kuondoka sehemu za Kefraya na Fouaa.

Aidha Vyombo vya habari vya huko vimesema, kikundi kinachoundwa na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, Iran na makundi ya upinzani ya Syria kitasimamia utekelezaji wa makubaliano hayo.

Josephine Charles........................                                       

 ____________________________________________________________


Bukola Saraki            
ABUJA
 
Rais wa Bunge la Seneti nchini Nigeria, Bukola Saraki, amefika kortini Abuja leo ambapo anakabiliwa na makosa 13 yanayohusu maadili.

Makosa hayo ni pamoja na kuhadaa, akitangaza mali yake pamoja na kukosa kutangaza mkopo, makosa ambayo ameyakanusha.

Imeelezwa kuwa Alikuwa ametarajiwa kufika kortini mara mbili awali lakini hakufika.
Kesi dhidi yake inaendeshwa na jopo la mahakama kuhusu maadili na inahusu makosa anayodaiwa kuyatenda alipokuwa gavana wa jimbo la Kwara kati ya mwaka 2003 na 2011.

Jopo hilo lilikuwa limetoa kibali cha kukamatwa kwake siku ya Ijumaa wiki iliyopita baada ya kukosa kufika kortini.

Aidha Bwana Saraki, amekuwa akijitetea na kushangaa ni kwa nini imechukua miaka 12 kutambua kwamba kulikuwa na kasoro katika karatasi zake za kutangaza mali yake na pesa anazodaiwa.

Josephine Charles..................                                                  

No comments: