Sunday, September 20

JESHI LA POLISI MKOANI DODOMA LIPO VIZURI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU MWEZI UJAO

JESHI la Polisi Mkoani hapa limesema katika kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wananchi wanapaswa kutii sheria, kanuni na taratibu za kampeni za uchaguzi bila kusubili shuruti.
 
Pia limesema limejipanga vizuri hivyo wananchi wasithubutu kufanya vurugu kwani hatua kali zitachukuliwa dhidi yao na kwamba wamejipanga vyema huku wakiwa na vifaa vya kutosha vya mawasiliano kama camera na vinasa sauti.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, david Misime aliyasema hayo wakati akiwasilisha mada ya majadiliano ya kudumisha, uzalendo,  amani, utulivu na usalama katika kipindi cha kampeni, uchaguzi, kupiga kura kutangaza matokeo kwa viongozi wa dini, vyama vya siasa serikali, taasisi, wazee maarufu na wadau mbalimbali.
Alisema ni jukumu la viongozi wa kisiasa kuwaelimisha wafuasi wao kuwa wanatakiwa kuhudhuria mikutano ya kampeni kwenda kusikiliza na sio kutoa maneno ya kashfa, uchochezi, kupandikiza chuki za kuzomea na kufanya fujo .
"Wakitoka kwenye mikutano, wanapokutana na na wanachama wa vyama vingine wasitumie maneno ya kashfa, kuwazomea, matusi, wasiwapige na wala wasiharibu mali zao kwani hayo yote ni kuvunja sheria za nchi na ni kosa la jinai", amesema Kamanda Misime.
Tunategemea hayo yafanyike kwa amani na kwa haki ili litakapokamilika tubaki na Dodoma yetu ikiwa na amani, utulivu na usalama," alisema na kuongeza ili hayo yaweze kutimia kila mmoja anapaswa kutii sheria, kanuni na taratibu za kampeni au uchaguzi bila shuruti.
Kwa upande wa viongozi wa dini, Misime alisema  kwa kuwa jamii inaamini yale wanayowafundisha  waendelee kuwasaidia kuwa pamoja na haki zao za kikatiba walizonazo ziambatane na wajibu wa kutii sheria.
Misime alisema pamoja na kuzingatia utii wa sheria pia wanapaswa kuwaelimisha walio chini yao ili waweze kutambua umuhimu wa kutii sheria bila shuruti kwnai kazi kazi ya uelimishaji ili iweze kuzaa matunda lazima ianze katika ngazi ya familia.
Akifungua semina hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Luteni Mstaafu Chiku Gallawa alihimiza viongozi hao kuhakikisha kuwa vurugu hazitokei kwenye uchaguzi mkuu na hata baada ya matokeo.
Gallawa alilaani kitendo cha wafuasi wa vyama vya kisiasa kuharibu mali za vyama vingine pamoja na uchanaji wa mapango ambapo alisema serikali haitavumilia vitendo kama hivyo kwani Tanzania ni nchi ya amani.
"Amani ikiondoka ni vigumu sana kuirejesha hivyo tunapaswa kila mmoja wetu bila kuangalia chama, kuhakikisha amani iliyopo inalindwa  sana," alisema.
 

No comments: