------------------------------ -----
MWENYEKITI WA CCM,
MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE,
MAKAMU MWENYEKITI WA CCM ZANZIBAR,
MHESHIMIWA DKT. ALI MOHAMED SHEIN,
MAKAMU MWENYEKITI WA CCM TANZANIA BARA,
NDUGU PHILIP MANGULA,
KATIBU MKUU WA CCM,
NDUGU ABDULRAHMAN KINANA,
NAIBU KATIBU MKUU WA CCM ZANZIBAR,
NDUGU VUAI ALI VUAI,
WAJUMBE WA KAMATI KUU YA CCM,
WAGENI WAALIKWA,
MABIBI NA MABWANA.
Assalam Aleykum,
Mheshimiwa
Mwenyekiti, awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu
kwa rehema na neema zake na kwa kutujaalia kukutana tena katika Mkutano
wetu huu adhimu tukiwa wazima wa afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwako Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM kwa kukiongoza Chama chetu kwa umakini, hekma, umahiri na weledi wa hali ya juu. Pia, nachukua fursa hii kumshukuru Makamu Mwenyeketi wa CCM Tanzania Bara na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar kwa bidii zenu, ushauri na utendaji wenu mzuri katika kukiendeleza na kukiimarisha Chama chetu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwa nafasi ya kipekee napenda kuwashukuru Katibu Mkuu wa
CCM na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, kwa juhudi zao kubwa za
kukiendeleza na kukiimarisha Chama chetu, hali ambayo inazidi kuongeza
imani kwa wananchi na kukijengea heshima kubwa chama chetu katika medali
ya siasa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Napenda kuchukuwa fursa hii kuwashukuru
Wajumbe wote wa Kamati kuu ya CCM kwa utekelezaji wa majukumu
katika kukisimamia, kukilinda na kukiendeleza chama chetu kwa mafanikio
makubwa katika maeneo yao ya kichama.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwa mara nyengine tena nachukua fursa hii kukupongeza wewe
Mwenyekiti ambae pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja
na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambae pia ni Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuzisimamia Serikali zetu zote
mbili katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha
miaka mitano iliyopita (2010-2015). Pia, nawashukuru Viongozi wote wa
Serikali zetu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi
wote wa Tanzania kwa ushiriki wao katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya
CCM ya Mwaka 2010 – 2015 kwa ufanisi na mafanikio makubwa.
UTANGULIZI:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye
muundo wa Umoja wa Kitaifa imetekeleza mipango mbali mbali ya maendeleo
kwa kuzingatia maagizo na malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha
Mapinduzi ya mwaka 2010 hadi 2015. Malengo hayo yamewekwa katika Sekta
ya Uchumi, Sekta za Uzalishaji Mali, Sekta za Miundombinu na Huduma za
Kiuchumi, Sekta za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Sekta za Huduma za
Kijamii pamoja na maeneo mengine ya kipaumbele.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imetekeleza majukumu yake kwa mafanikio makubwa.
Mafanikio hayo ni pamoja na kuendelea kwa hali ya amani na utulivu hapa
nchini; kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka vianzio
mbali mbali kufuatia juhudi zilizofanywa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuziba mianya ya uvujaji wa mapato,
kukua na kuimarika kwa utawala bora unaotilia mkazo suala
la uwajibikaji ndani ya sekta ya umma na kuimarika kwa mshikamano
wa wananchi.
HALI YA SIASA:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015 hali ya kisiasa
Zanzibar kwa kiasi kikubwa imekuwa ya amani na tulivu, hakukuwa na
matukio makubwa ya uvunjifu wa amani. Hali hii inatokana na wananchi
wengi kuzidi kuelewa umuhimu wa kudumisha amani na utulivu pamoja na
kushirikiana na Serikali kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla. Matukio
muhimu ya kisiasa yalijitokeza katika kipindi hiki ni kufanyika chaguzi
ndogo mbili kwa nafasi za Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na chaguzi
tatu za Udiwani ambazo kwa nafasi zote hizo CCM
ilishinda.
Pia, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeendesha chaguzi ndogo ya nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Chambani. Vile vile, katika kipindi hicho, nchi yetu iliadhimisha sherehe za kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar sherehe ambazo zilifana sana.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, ingawaje hali ya amani na utulivu iliendelea kutawala
nchini katika kipindi chote cha taarifa hii hata hivyo kulijitokeza
baadhi ya matukio yaliyoashiria uvunjifu wa amani. Matukio hayo ni
pamoja na kuuawa kwa askari wa Jeshi la Polisi na kiongozi mmoja wa
kidini, kumwagiwa tindikali kwa viongozi wa dini na Serikali, na wageni
wakitalii. Pia, kulitokea mripuko uliosadikiwa kuwa ni bomu na
kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi watu wengine katika eneo la
Darajani.
Aidha, vilijitokeza vikundi vilivyoandaa mihadhara waliyodai kuwa ya kidini na kufanya maandamano bila ya kupata kibali na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali za Serikali, mali za wananchi pamoja na nyumba za ibada. Vile vile
Maskani
kadhaa na matawi ya CCM yalichomwa moto. Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar chini ya uongozi wenye hekima na busara wa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Ali Mohamed Shein
ilifanikiwa kudhibiti vurugu hizo kwa kuwakamata waliohusika
na kuwafikisha katika vyombo vya kisheria
HALI YA KIUCHUMI:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2010-2015)
uchumi wa Zanzibar umeendelea kuonyesha mwenendo mzuri ambapo ukuaji wa
Pato la Taifa umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka kutoka asilimia 6.4
mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 7.4 mwaka 2015.
Aidha,
mapato ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yameonyesha kuongezeka
kutoka TZS Bilioni 181 kwa mwaka 2010/11 hadi kufikia TZS Bilioni 330
mwaka 2014/2015 sawa na ongezeko la asilimia 82. Ongezeko hilo
limetokana na kuimarika kwa Sekta ya Kilimo, Misitu na Uvuvi,
Sekta
Ndogo ya Uzalishaji Viwanda, Sekta ya Huduma inayojumuisha Sekta Ndogo
ya Hoteli na Mikahawa, na kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaoingia
nchini. Ongezeko hilo limechangiwa kwa kiasi kutokana na
juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuimarisha ukusanyaji wa
mapato na kuziba mianya inayosababisha uvujaji wa mapato. Mheshimiwa
Mwenyekiti, hali ya mfumko wa bei kwa upande wa Zanzibar imeshuka
kutoka asilimia 6.1 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 5.6 mwaka 2014,
hali hii imetokana na juhudi za Serikali katika kudhibiti mfumko huo wa
bei ikiwemo kutoa ruzuku za pembejeo kwa wakulima ambako kulipelekea
kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula.
Aidha, Serikali imetoa misamaha ya kodi kwa bidhaa muhimu za chakula kama vile sukari, unga na mchele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza kutekeleza ahadi ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015 ya kuendeleza Maeneo Huru ya Kiuchumi ya Fumba. Katika utekelezaji wa ahadi hii, Serikali imechukuwa hatua mbali mbali ikiwa ni pamoja na kutayarisha Mpango Mkuu wa Matumizi ya Ardhi Fumba, upimaji na utayarishaji wa mchoro wa ramani ya eneo hilo. Jumla ya hekta 3,000 zimepimwa na kugaiwa kwa matumizi tofauti ambapo hekta 743 zimetengwa kwa ajili ya uwekezaji wa shughuli za kibiashara, hekta 1,310 kwa ajili ya vijiji vya asili na
makaazi na hekta 946 kwa ajili ya eneo la akiba.
Pia, Serikali imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa njia kuu ndani ya eneo la uwekezaji Fumba yenye urefu wa kilomita 10 kwa kiwango cha lami. Aidha, Serikali imekamilisha mazungumzo na Mwekezaji wa Kampuni Mama ya
Bakhressa
Group juu ya kushirikiana katika uwekezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Mji wa
Kisasa wa Fumba (Fumba Bay Satillite City). Kwa sasa kiwanda kikubwa
cha usarifu maziwa cha Azam Dairy Milk na Zanzibar Fiber Glass tayari
vimeanzishwa na vinaendelea na kazi na miradi mingine ya huduma na
nyumba za makaazi imo katika hatua za awali.Kutekelezwa kwa miradi ya
aina hii katika eneo hilo la Fumba kunatarajiwa kuzalisha ajira zaidi
kwa wananchi pamoja na kukuza Pato la Taifa.
SEKTA ZA UZALISHAJI MALI:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Sekta za Uzalishaji Mali zinajumuisha kilimo, ufugaji,
uvuvi, maliasili, utalii, viwanda na biashara na Vyama VyaUshirika.
KILIMO:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Sekta ya Kilimo ni mojawapo ya sekta muhimu sana kwa uchumi
wa Zanzibar ambapo inatoa mchango wa moja kwa moja katika kujikimu
kimaisha. Pia, sekta hii ni muhimu kwa upatikanaji wa uhakika wa chakula
katika ngazi ya familia na Taifa na inasaidia kuimarisha lishe na afya
za wananchi walio wengi mijini na vijijini.
Aidha,
inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wa
Zanzibar wanategemea Sekta ya Kilimo kwa kuwapatia ajira na
kipato. Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la karafuu ndilo linalochangia kwa
kiasi kikubwa katika mchango wa sekta ya kilimo katika pato la Taifa.
Zao hilo pia ndilo linaloingizia nchi yetu kiasi kikubwa cha fedha
za kigeni. Katika jitihada za kuliendeleza zao la karafuu,
Serikali imeendelea kuongeza uzalishaji wa miche ya mikarafuu kutoka
mwaka hadi mwaka. Kutokana na juhudi mbali mbali za Serikali na
wakulima, uzalishaji wa karafuu umeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kunakosababisha
kutokuwa na uhakika wa upatikanaji wa mvua, Serikali kwa kushirikiana na
wadau wa Maendeleo imeendelea kuchukua jitihada za kuimarisha kilimo
cha umwagiliaji maji kinachoongeza tija na uzalishaji na kuwaongezea
kipato wakulima wetu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kuongeza kasi ya maendeleo ya kilimo, Serikali
kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Kizimbani imeendelea kufanya tafiti
mbali mbali za kilimo pamoja na kusambaza matokeo ya tafiti hizo kwa
wakulima na wadau wengine wa kilimo. Miongoni mwa tafiti zilizofanywa ni
pamoja na tafiti ya zao la mpunga, mazao ya mizizi na matunda na
utafiti wa matumizi ya mbolea mpya. Aidha, Serikali imenunua vifaa
mbali mbali vya kilimo ikiwemo matrekta na mashine za kuvunia mpunga
pamoja na kuyafanyia matengenezo matrekta ya zamani. Serikali pia
imezidi kukiimarisha Chuo cha Kilimo Kizimbani ili kiweze kutoa mafunzo
ya kilimo na mifugo kwa wanafunzi, wakulima pamoja na wadau wengine wa
kilimo.
UFUGAJI:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imetekeleza mpango wake wa kuendeleza ubora wa
mifugo kwa kupata mbegu bora za mifugo zenye manufaa zaidi kwa wafugaji,
kutoa elimu kwa watoa huduma za msingi, madaktari wasaidizi na wafugaji
juu ya namna ya kuendeleza ufugaji
bora, kukuza fursa za masoko na kuimarisha huduma za kinga na tiba
kwa mifugo. Matokeo ya jitihada hizo yemepelekea kuongezeka uzalishaji
wa mazao ya mifugo.
UVUVI NA MAZAO YA BAHARINI:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kuendeleza Sekta ya Uvuvi, Serikali imeendelea na
jitihada zake za kuwasaidia na kuwaendeleza wavuvi wadogo wadogo kwa
kuwapatia zana bora na za kisasa, kuwapatia taaluma bora ya uvuvi
unaozingatia uhifadhi wa mazingira ya bahari, kuwajengea miundombinu ya
masoko na uhifadhi wa samaki, kuwapatia taaluma ya ufugaji wa samaki na
kuwaongezea uwezo juu ya uzalishaji bora wa zao la mwani. Kutokana na
juhudi hizi uzalishaji wa samaki umeongezeka kwa kiasi kikubwa kwa
Unguja na Pemba. Aidha, katika kupambana na uvuvi haramu na uharibifu
wa mazao ya baharini, Serikali imeendelea kufanya doria na kutoa mafunzo
kwa vikundi vya uvuvi, wananchi na Kamati za Uvuvi pamoja na kutoa
leseni za uvuvi.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, uzalishaji wa zao la mwani umekuwa ukiwasaidia wananchi
hasa kinamama katika kuwaongezea kipato chao. Katika kulifahamu hilo,
Serikali imeendeleza tafiti juu ya zao la mwani, imetoa vifaa pamoja na
kuwapatia soko la uhakika wakulima wa zao hilo.
MALIASILI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufahamu umuhimu wa misitu na maliasili zisizorejesheka, Serikali imeendelea na udhibiti na uhifadhi wa maliasili zikiwemo rasilimali za misitu pamoja na maliasili zisizorejesheka kwa kutoa elimu na kushajiisha jamii juu ya uhifadhi wa rasilimali hizo. Aidha, Serikali imekuwa ikichukua jitihada kubwa juu ya suala zima la ushajiishaji jamii katika muendelezo wa kupanda
na kuitunza miti.
UTALII:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali imeendelea na juhudi mbali mbali zakuimarisha
Sekta ya Utalii kwa kuifanyia mapitio makubwa Sheria ya Utalii kwa
lengo la kuzidisha kasi ya usimamiaji wa masuala ya utalii, kuanzisha
Maabara ya Utalii yenye lengo la kuibua mikakati imara ya kupanua wigo
katika sekta hii muhimu pamoja na kuitangaza Zanzibar kiutalii katika
nchi mbali mbali. Aidha, Serikali imeendelea na mikakati yake ya
kuimarisha sekta hii. Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na
uimarishaji wa miundombinu ya utalii, kuimarisha vivutio vya
utalii na kukiboresha Chuo cha Maendeleo ya Utalii.
VIWANDA NA BIASHARA:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kusimamia utekelezaji wa Sera ya Uendelezaji wa
viwanda vidogo vidogo na vya kati, Serikali imefanya ukarabati mkubwa wa
Kiwanda cha Sukari kilichopo Mahonda. Vle vile Serikali imeshajihisha
sekta binafsi kuwekeza katika viwanda ambapo kiwanda kikubwa cha maziwa
(Azam Diary Factory) kimefunguliwa rasmi na kimeanza kazi za uzalishaji
na usambazaji wa maziwa ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kuliendeleza zao la karafuu, Serikali imechukua
hatua za kuilinda na kuipa hadhi zaidi karafuu yetu pamoja na kuitangaza
Zanzibar ulimwenguni kupitia bidhaa nyengine za viungo zikiwemo
mdalasini, pilipili hoho, na pilipili manga ambapo kazi hii inatekelezwa
kupitia mradi wa Tasnia Malibunifu (Branding). Pia, Serikali imeunda
Taasisi ya Viwango ya Zanzibar (ZBS) katika kusimamia ubora wa bidhaa
zinazozalishwa na kuingizwa nchini.
VYAMA VYA USHIRIKA:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitano Serikali imeendelea na
juhudi zake za kuimarisha na kuendeleza vyama vya ushirika kwa kutoa
mafunzo juu ya ushindani, ubunifu na ujasiriamali kwa walengwa. Aidha,
Serikali katika hatua za utunzaji wa rasilimali na hesabu za ushirika
imefanya ukaguzi wa hesabu za vyama vya ushirika mbalimbali kwa Unguja
na Pemba.
MIUNDOMBINU YA KIUCHUMI:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, miundombinu ya kiuchumi inajumuisha barabara viwanja vya
ndege, usafiri wa baharini, umeme na bandari. Kutokana na umuhimu huo
Serikali imetekeleza yafuatayo kisekta.
BARABARA:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara za Unguja na
Pemba ili ziendelee kupitika kwa wakati wote na kuwarahisishia wananchi
usafiri. Jumla ya kilomita 181.7 za barabara kwa Unguja na Pemba
zimekamilika. Vilevile, barabara zenye urefu wa kilomita 36.5
zilizojengwa kwa kiwango cha kifusi kwa Unguja na Pemba zimekamilika.
Pia, barabara zenye urefu wa kilomita 80.5 zinaendelea kujengwa kwa
kiwango cha lami zinaendelea kujengwa kwa Unguja na Pemba.
Usafiri wa Baharini:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kuimarisha miundombinu ya Usafiri wa Baharini,
Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya AZAM MARINE imejenga majengo ya
kuhudumia abiria katika Bandari ya Malindi. Aidha, Serikali
imekamilisha matengenezo makubwa ya gati ya Mkoani Pemba na kuondoa tatizo la kutuama kwa maji juu ya gati hiyo.
Mheshimwa Mwenyekiti, katika kuwaondolea usumbufu wa usafiri wananchi wetu na watumiaji wengine baina ya visiwa vyetu na maeneo mengine ya mwambao wa Afrika Mashariki, Serikali kupitia Shirika la meli inaendelea na ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kuchukua abiria 1200 na mizigo tani 200. Meli hiyo inatengenezwa nchini Korea ya Kusini na inatarajiwa kuingia nchini mwishoni wa mwezi Julai, 2015.
Usafiri wa Anga:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kuimarisha huduma za Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa
cha Abeid Amani Karume, Serikali imeendelea na kazi ya kujenga uzio
wenye urefu wa kilomita 11.9. Aidha, Serikali inaendelea
na ujenzi wa jengo jipya la abiria lenye ukubwa wa mita za
mraba 25,000. Jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria
1,600,000 kwa mwaka. Serikali inaendelea kufanya marekebisho na
kuongeza eneo
la kuegeshea ndege lenye ukubwa wa mita za mraba 37,000.
Marekebisho hayo yatabadilisha mfumo wa uegeshaji wa ndege kubwa kutoka
mbele ya jengo (airside) na badala yake kuegesha upande wa kusini ya
jengo.
UMEME:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Nishati ya Umeme ni muhimu katika kujenga msingi wa uchumi
wa kisasa wa Taifa linalojitegemea. Katika kutekeleza azma hiyo Serikali
imejenga njia ya umeme inayopita chini ya bahari
kutoka Ras Kiromoni Tanzania Bara hadi Fumba Unguja na inayotoka
Tanga hadi Pemba. Mpango huu umetuwezesha kupata kiwango cha umeme
kutoka “Megawatt” 45 na kufikia 145 kwa Unguja na kwa upande wa
Pemba “Megawati” 20 zimeongozeka. Pia Serikali imeendelea na
uimarishaji wa vituo vya usambaziji umeme katika maeneo mbali mbali na
kutilia mkazo usambazaji wa umeme mijini na vijijini. Katika kuendeleza
juhudi za utafiti wa vyanzo vya nishati mbadala ya umeme ukiwemo umeme
wa jua, mawimbi ya bahari, upepo na gesi asilia, Serikali imeyakagua
upya na kuyafanyia uhakiki maeneo yote ambayo yalifanyiwa utafiti wa
awali na kupendekezwa na wataalamu kutoka EU ili kutumika kwa ajili ya
nishati mbadala kabla ya kuanza hatua ya utekelezaji. Pia, Serikali
imeendelea kuliimarisha Shirika la Umeme (ZECO) ili lizidi kujiendesha kibiashara na kutoa huduma bora wananchi.
ARDHI:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali imeandaa Sera ya Ardhi ambayo itasimamia matumizi
bora ya ardhi kwa matumizi ya sasa na vizazi vijavyo. Aidha, Serikali
imefanya upitiaji na utayarishaji wa Mpango Mkuu wa Kitaifa wa Matumizi
Bora ya Ardhi wa Zanzibar (National Land Use Plan). Vile vile, Serikali
inaendelea na kazi ya usajili wa ardhi,
kuwaelimisha wananchi juu matumizi bora ya ardhi pamoja na kuziimarisha
na kuanzisha Mahakama za Ardhi katika kila Mkoa na kuongeza idadi ya
Mahakimu kwa lengo la kupunguza migogoro ya ardhi katika maeneo yao.
MAZINGIRA:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali bado inaendelea na mikakati ya uthibiti na
uhifadhi wa mazingira kwa kuandaa, kutekeleza na kusimamia mipango mbali
mbali ya uhifadhi wa mazingira katika maeneo ya ardhi, bahari na ukanda
wa pwani. Aidha, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali
imefanya mapitio na ukaguzi wa miradi inayohusiana na mazingira ili
kupata tathmini ya athari za kimazingira. Vile vile Serikali imezindua
kikosi kazi cha udhibiti wa uharibifu wa mazingira katika visiwa vya
Zanzibar. Pia, Serikali imefanya mapitio ya Sera ya
Mazingira ya mwaka 1992 na kuzindua Sera ya Mpya ya Mazingira ya
mwaka 2013 ambayo inatoa miongozo kwa shughuli za uhifadhi wa mazingira.
HUDUMA ZA JAMII:
ELIMU:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali imetoa kipaumbele kwa Sekta ya Elimu kwa sababu
ndio msingi wa maendeleo ya jamii na Taifa kwa jumla.Katika kulitilia
mkazo suala hilo, Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kuboresha
elimu kama ifuatavyo:-
Elimu ya Maandalizi:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kuendeleza juhudi za kuongeza ushiriki wa wanafunzi
katika ngazi ya maandalizi, idadi ya Skuli za Maandalizi imeongezeka
hadi kufikia 270 mwaka 2015 kutoka 238 mwaka 2010 hali ambayo ongezeko
la wanafunzi 29,732 mwaka 2010 na kufikia wanafunzi 38,808 mwaka 2015.
Kwa upande wa Elimu ya Msingi, Serikali kwa kushirikiana na wananchi
imeendelea kujenga skuli za msingi kwa sasa
jumla ya skuli 370 mwaka 2015 kutoka 299 mwaka 2010. Aidha,
Serikali imekamilisha ujenzi wa skuli 19 za sekondari Unguja na Pemba
kwa asilimia 100 na tayari skuli hizo zinatumika. Pia Serikali imeongeza
juhudi za kuzipatia vifaa vya kufundishia na kujifunzia skuli zote za
Maandalizi, Msingi na Sekondari. Pia, Serikali inaendelea na juhudi za
kuimarisha masomo ya Sayansi na Hisabati kwa kuwapatia mafunzo kazini
Walimu wa masomo hayo, Walimu Wakuu, Maafisa wa Elimu wa Wilaya na
Mikoa. Vile vile, Serikali inaendelea na jitihada katika kutoa elimu ya
watu wazima, hali ambayo imepelekea kupungua kwa idadi ya wanakisomo kwa
kiasi kikubwa.
Huduma za maktaba:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kuimarisha huduma za maktaba, Serikali imekamilisha
ujenzi wa Maktaba Kuu ya Zanzibar na kujenga Maktaba mpya kwa upande wa
Pemba. Aidha, Serikali imeendelea kuzipatia vitabu na huduma nyengine za
kimaktaba ili kuziwezesha kutoa huduma kwa ufanisi. Pia Serikali
kupitia Shirika la Huduma la Maktaba limeendesha mafunzo ya ukutubi kwa
walimu wa skuli 44 za Unguja na 40 za Pemba ili wapate taaluma sahihi
juu ya namna bora ya kutoa huduma za maktaba na kukuza maendeleo ya
elimu. Aidha, Serikali imeanzisha utaratibu wa kuwa na maktaba za jamii
ili ziweze kutoa huduma kwa jamii kwa ukaribu zaidi.
Elimu ya Juu:
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutilia mkazo suala la elimu ya juu nchini, Serikali imekamilisha ujenzi wa Chuo Kikuu Cha Taifa SUZA, Tunguu. Ujenzi huo umekamilika kwa majengo manne (4) na kuweka vifaa kwa ajili ya chuo hicho. Aidha, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2010 – 2015), Serikali imezidi kuongeza fursa za elimu ya
juu kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma ndani na nje ya nchi.
Vile
vile, Serikali imeboresha mazingira ya wawekezaji wa Sekta Binafsi
kuendelea kuekeza katika elimu ya juu. Chuo kikuu cha Zanzibar
kinaendelea kutoa mafunzo mbali mbali katika Shahada ya Kwanza na
Shahada ya Pili. Chuo cha Elimu Chukwani kimepandishwa hadhi na kuwa
Chuo Kikuu kamili (Al-Ssumait University) na hivyo kukiwezeshakutoa
shahada za juu.
Mafunzo ya Ualimu:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kuimarisha mafunzo ya ualimu, Serikali imeandaa
Rasimu ya Sera ya Mafunzo ya Ualimu Kazini na imefanya mapitio ya Mtaala
wa Diploma ya Msingi. Mtaala huo umeingiza masomo mapya yakiwemo ya
habari na mawasiliano, mafunzo ya amali, uongozi na michezo. Aidha,
Serikali imeendesha mafunzo kazini kwa walimu wa Skuli za Msingi na
Sekondari kwa masomo ya Sayansi na Hesabati, kompyuta na somo la
Kiingereza pamoja na mbinu bora za kufundishia kwa njia ya mtandao.
Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Amali:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutoa elimu ya amali kupitia Vituo vya
Mafunzo ya Amali vya Mkokotoni, Mwanakwerekwe na Vitongoji. Vituo hivyo
vinatoa mafunzo ya fani mbali mbali za ufundi zikiwemo useremala,
ushoni, uhunzi, upishi, uchoraji na uandishi wa alama, uashi, ufundi
bomba, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, huduma za chakula na
vinywaji, ufundi magari, umeme na ufundi wa mafriji na viyoyozi. Aidha,
Serikali imeendelea kukiimarisha Chuo cha Ufundi Karume kwa ujenzi wa
Madarassa na Mabweni ya wanafunzi, ukarabati wa mfumo wa maji na umeme
kwa majengo yote ya chuo pamoja na kukipatia vifaa vya mawasiliano ili
kukiwezesha kwenda sambamba na ulimwengu wa sayansi na teknolojia. Vile
vile, Serikali imeiendeleza na kuimarisha Skuli ya Ufundi Kengeja huko
Pemba.
SEKTA YA AFYA:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali
imejikita katika kusimamia utekelezaji wa sera na programu mbali mbali
zinazohusiana na sekta ya afya. Huduma za Kinga na Tiba:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kuendeleza huduma ya kinga na tiba, Serikali
imefanya utafiti juu ya kuangalia kiwango cha sababu hatarishi
zinazopelekea kupata maradhi yasiyo ya kuambukiza. Matokea ya utafiti
huo yameonesha idadi kubwa ya jamii inasumbuliwa na tatizo la uzito
mkubwa (Obesity). Serikali kwa kushirikiana na Jumuiya ya Watu
wanaoishi na Kisukari, imeshajiisha jamii kuanzisha vikundi vya mazoezi
katika Wilaya zote za Unguja na Pemba. Aidha, Serikali inaendelea
kuchukua juhudi mbali mbali za kukuza uelewa kwa jamii juu ya kujikinga
na maradhi ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.
Vilevile,
Serikali inaendelea kutoa huduma za tiba kwa magonjwa mbali mbali
yakiwemo maradhi ya moyo, kisukari na mengineyo kwa wananchi wake
kupitia hospitali na vituo vya afya kwa kipindi chote cha miaka mitano
iliyopita.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali inaendelea na kampeni za kupunguza na kudhibiti
malaria Zanzibar. Katika Mpango huo ujulikanao kama “Maliza Malaria
Zanzibar”, Serikali imefanikiwa kupunguza ugonjwa wa Malaria
katika jamii kutoka asilimia 0.06 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 0.03
mwaka 2013. Katika kupambana na ugonjwa wa UKIMWI, Serikali imeimarisha
huduma za tiba na huduma za kuzuia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto.
Aidha, Serikali imeimarisha vituo vya ushauri nasaha na upimaji wa VVU
kwa kuvipatia nyenzo za kufanyia uchunguzi. Vile vile, Serikali
imeendelea kutoa elimu na tiba kwa maradhi nyemelezi
kama vile kifua kikuu na ukoma ili kupunguza maambukizi zaidi.
Huduma bora za Afya kwa wananchi wote:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kuhakikisha kuwa hospitali zetu zote zinatoa huduma
bora za afya kwa wananchi wetu, Serikali inaendelea na mipango yake ya
kuzipandisha daraja hospitali zake za Unguja na Pemba. Katika kutekeleza
mkakati huu, Serikali imeziongezea majengo pamoja na kuzipatia vifaa
vya kisasa Hospitali ya Mnazimmoja ili ifikie hadhi ya Hospitali ya
Rufaa, hospitali ya Abdallah Mzee Mkoani ili ifikie hadhi ya hospitali
ya Mkoa na Hospitali za Wete, Kivunge na Makunduchi ili zifikie hadhi ya
Hospitali za Wilaya. Aidha, Serikali meendelea kuviendeleza vituo vya
afya vikiwemo vya daraja la kwanza na daraja la pili ambavyo vinatoa
huduma za ziada kama vile huduma za kuzalisha, maabara na huduma za
meno. Vile vile, Serikali imeifanyia mapitio Sera ya Afya ya mwaka 1999
na kuwa na Sera mpya ya mwaka 2011 pamoja na Sheria ya Afya ya Jamii
ambazo zinakwenda sambamba na mahitaji pamoja na mikataba ya kitaifa,
kikanda na kimataifa katika utoaji wa huduma za afya nchini.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo
vya afya unakuwa wa kuridhisha kwa wananchi, Serikali inaendelea kutoa
huduma za dawa bila ya malipo katika hospita i zote
na vituo vya afya. Vituo vyote hivi vinafaidika na upatikanaji wa dawa
chini ya mpango maalum ujulikanao kama “Zanzibar Integrated Logistic
System”. Aidha, Serikali imejenga Bohari Kuu ya Madawa iliyopo Maruhubi
ambayo itarahisisha kupata na kutoa taarifa za hali ya upatikanaji wa
dawa kutoka hospitali na vituo vya afya mbali mbali
nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja wapo katika jambo muhimu la upatikanaji wa huduma ya afya kwa wananchi ni kuwa na madaktari na watoa huduma wenye uwezo mzuri wa kazi hiyo. Katika kuhakikisha kuwa azma hii inafikiwa,
Serikali
inaendelea kuwajengea uwezo madaktari na watoa huduma wa hospitali na
vituo vya afya kwa kuwapeleka masomoni katika vyuo mbali mbali vya ndani
na nje ya nchi. Hatua hii imeweza kutupatia madaktari na watoa huduma
wenye ufanisi zaidi kwa wananchi wetu. Aidha, Chuo cha Taaluma cha
Sayansi za Afya kinaendelea kutoa taaluma za afya kwa kiwango cha
Stashahada katika fani mbali mbali. Vile vile, Serikali kwa kushirikiana
na Serikali ya Cuba imewasomesha wanafunzi 38 wa kada ya Udaktari,
ambao tayari wamemaliza masomo yao, hivyo kupata
madaktari wengine wazalendo 38 idadi hiyo imewezesha madaktari
wote wanaotoa huduma Zanzibar kufikia 142, kati ya hawa madaktari 40
ni madaktari wa kigeni kutoka Cuba na China hali ambayo imepelekea
kwa sasa kuwa na uwiyano wa daktari mmoja kuhudumia wastani wa
wagonjwa 9,708.
Huduma Za Tiba Asili:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kusimamia matumizi sahihi ya Tiba Asili, Serikali
kwa kushirikiana na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala imeelimisha
jamii kupitia vyombo mbali mbali vya habari, kutumia vipeperushi pamoja
na kufanya mikutano. Pia, Baraza limefanikiwa kutengeneza Kanuni
(regulations) za Tiba Asili na kutoa elimu kwa
waganga. Sambamba na hayo, Baraza limeweza kusajili waganga,
waganga wasaidizi, kliniki za tiba asili na tiba mbadala, viringe au
sehemu wanazofanyia na maduka ya dawa za asili baada ya kutimiza
masharti ya sheria za Baraza. Aidha, Serikali imefanya uchunguzi wa
sampuli za dawa asilia chini ya usimamizi wa Maabara ya Bodi ya Chakula
na Madawa. Vile vile, katika kuhakikisha Baraza la Tiba Asili
linafanya kazi zake vizuri na ipasavyo limejenga uhusiano mzuri kati
ya madaktari wa kisasa (Biomedical Practitioners) na waganga wa asili
(Traditional Healers).
MAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua za kuendeleza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi, Serikali imeendelea na uchimbaji wa visima na ulazaji wa mabomba makubwa katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba ambapo utekelezaji wa hatua hii umefikia asilimia 96.15 kwa Unguja na asilimia 96.26 kwa Pemba. Pia Serikali imesambaza pampu mpya katika maeneo mbali mbali ya mijini na vijini ambapo kwa sasa mradi huu mefikia asilimia 94 ya utekelezaji. Aidha, mradi wa usambazaji maji safi na salama katika Mkoa wa Mjini Magharibi
uliojumuisha ujenzi wa matangi mawili umekamilika.
MAKAAZI:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali kwa kuzingatia agizo la Ilani ya Uchaguzi ya CCM
(2010-2015) imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Nyumba
na Sheria ya Shirika la Nyumba la Zanzibar ya mwaka
2014 imeshapitishwa na Baraza la Wawakilishi. Aidha, Serikali imekamilisha ujenzi wa Nyumba ya Maendeleo Bambi (Mpapa) ambapo fleti 24 zimekabidhiwa kwa wananchi wakati wa Sherehe za Maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vile vile Serikali inaendeleza Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao ni hazina kubwa na kivutio cha historia ya Zanzibar. Hivyo basi, Serikali kwa kushirikiana na watu binafsi inaendelea kuulinda, kuuhifadhi na kutumika kama kivutio cha utalii na kubakisha dhana ya urithi wa Dunia.
MAENEO MENGINE YA KIPAUMBELE:
Utamaduni na Michezo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, utamaduni ni moja kati ya mambo muhimu katika Taifa lolote duniani, kwa kuzingatia hilo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeifanyia mapitio Sera ya Utamaduni ili iendane na wakati kwa kuihusisha Sekta ya Utalii na Utamaduni. Aidha, katika kuufanya utamaduni uwe na tija zaidi, Serikali imekamilisha mchoro wa ramani ya
utamaduni
katika Shehia za Unguja na Pemba. Pia, Serikali imekamilisha utafiti wa
Urithi wa Utamaduni Usioshikika katika mikoa yote ya Unguja na Pemba na
hatimaye kuhifadhiwa na kutangazwa kimataifa kwa kuingizwa katika
orodha ya “UNESCO” ya Utamaduni uliohifadhiwa. Vile vile, Serikali
imechukua hatua za kuzikagua kazi za sanaa kwa lengo la kulinda na
kuhifadhi mila na silka za Wazanzibari. Pia, imeandaa makamusi ya
lahaja ya Kipemba, Kimakunduchi na Kitumbatu kwa lengo la kuendeleza
lahaja hizo.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kuendeleza michezo kwa faida ya vijana wetu na Taifa
kwa ujumla, Serikali imeifanyia mapitio Sera ya Michezo ili iwe
muongozo kwa shughuli zote za michezo nchini. Aidha, Serikali
imeufanyia matengenezo na marekebisho makubwa uwanja wa Gomabani
Pemba ili kuuwezesha uwanja huo kukidhi haja ya mashindano ya kimataifa
ya mpira wa miguu. Vile vile, Serikali kwa kushirikiana na Serikali
ya Japan imejenga ukumbi wa Zanzibar Budocan ndani ya Uwanja wa Amaan
na uwanja huo tayari umeanza kutumika kwa michezo ya judo, karati
na michezo mingine ya ndani inayolingana na hiyo. Sambamba na
hayo Serikali ya mekamilisha mradi wa ujenzi wa studio ya kisasa
ya kurikodia nyimbo na michezo ya kuigiza kwenye jengo la zamani
la Utangazaji la Sauti ya Tanzania Zanzibar baada ya jengo hilo
kufanyiwa matengezo makubwa. Tayari Serikali imenunua na kufunga vifaa
vipya kwa ajili ya studio hiyo ambavyo vimegharimu jumla ya shilingi
291,534,000.
Vyombo vya habari:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kuhakikisha wananchi wetu wanapata habari kwa wakati
na zenye uhakika, Serikali imetunga Sheria Namba 4 ya mwaka 2013 ya
kuunda Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), Sheria hiyo tayari
imepitishwa na Baraza la Wawakilishi na imeanza kufanya kazi. Sambamba
na hilo Serikali imeandaa na kusimamia utekelezaji wa Sheria ya vyombo
vya habari, kanuni na miongozo kwa lengo la kuleta ufanisi katika
mageuzi ya mfumo wa utangazaji kutoka Analogi kwenda Digitali. Aidha,
Serikali imeweza kufanya mageuzi
makubwa katika vyombo vya habari kwa kuvipa uhuru na haki ya
kuhoji, kutafuta, kupokea na kuchapisha habari na maoni bila ya woga.
Vile vile kwa lengo la kupanua misingi ya demokrasia ya habari,
Serikali imeshajiisha wawekezaji kuwekeza katika Sekta ya habari na
tayari vituo vya Redio vinne (4) na Televisheni vitano (5) vimeazishwa
katika kipindi cha 2010-2015.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, kufuatia mafanikio makubwa ya vyombo vya habari vya
Serikali, Shirika la Magazeti la Zanzibar limeweza kuongeza maeneo ya
usambazaji kwa Zanzibar na Tanzania Bara mjini na vijijini.
Pia Serikali imekuwa ikitoa miongozo mbali mbali kwa vyombo vya
habari kuzingatia maadili ya uandishi wa habari na pia kuheshimu na
kulinda maslahi na uhuru wa raia wa kuishi pamoja na haki za faragha.
Vile vile, Tume ya Utangazaji imeanzisha mfumo wa ufuatiliaji
vipindi (Monitoring System) ambapo hivi sasa vipindi vyote
inarikodiwa, kuhifadhiwa na kufuatiliwa. Aidha, katika kipindi cha 2010
hadi 2014, waandishi 42 wameweza kupatiwa mafunzo katika ngazi tofauti
zikiwezo Stashahada, Shahada ya Kwanza na Shahada ya Uzamili. Vile
vile, taaluma mpya ya teknolojia ya digitali imetolewa kwa
mafundi, watayarishaji vipindi na viongozi wa vituo vya utangazaji vya
Serikali na Binafsi vilivyopo Zanzibar.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali imeviimarisha Vyombo vya Habari vya Zanzibar kwa
kuvinunulia vifaa mbali mbali vya kisasa vinavyotumia teknolojia ya
digitali. Aidha, Serikali imeweza kuimarisha kazi za utangazaji kwa
kuhamisha mnara wa masafa ya kati (medium waves) kutoka Chumbuni kwenda
Bungi. Pia, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Watu
wa China imefanya ukarabati wa mnara wa mawimbi mafupi
(short wave).
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kutekeleza agizo la Ilani ya Uchaguzi ya CCM
(2010-2015) ya uendelezaji wa taaluma ya habari, Serikali imekiimarisha
Chuo cha Uandishi wa Habari kwa kuweka vifaa pamoja na kuajiri walimu
wenye ujuzi ili kuweza kutoa wahitimu wenye uwezo mzuri wa tasnia ya
habari. Vile vile, Chuo kimeweza kutengeneza nyaraka mbali mbali za
kitaalamu ikiwemo Kitabu cha Miongozo wa Shughuli za Chuo (Prospectus),
Mpango Mkakati (Strategic Plan) na Vipeperushi.
Pia,
Chuo kimeweza kuanzisha mafunzo ya lugha ya Kichina kwa kushirikiana na
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. Sambamba na hayo, Chuo kimekuwa
na ushirikiano wa karibu na Redio ya Kimataifa ya Deutsche Welle (DW) ya
Ujerumani ambayo imekuwa ikisaidia kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi
kwa kuwapatia mafunzo mbali mbali.
Majanga na huduma za uokozi:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kushughulikia masuala ya majanga na maafa, Serikali
imeandaa Sera ya kukabiliana na maafa, na Mpango wa Dharura wa Kujiandaa
na Kukabilana na Maafa. Vile vile, Serikali imeandaa Muongozo wa
Ufuatiliaji na Tathimini pamoja na Mkakati wa Mawasiliano wakati wa
Maafa. Aidha, elimu ya kukabiliana na maafa kwa ajili ya kujenga uelewa
kwa jamii juu ya majanga na maafa imetolewa katika ngazi ya Shehia,
Wilaya na Taifa. Kutokana na elimu hii Kamati za maafa za Shehia
zimeundwa katika Shehia za Unguja na Pemba. Aidha, Serikali imeweza
kukiimarisha Kikosi Maalum cha Uokozi na Uzamiaji cha (ZARDEC) kwa
kuwashirikisha katika shughuli mbali mbali za kukabiliana na maafa
pamoja na kuhamasisha vikosi vyengine vidogo vidogo kuanzisha
Jumuiya za pamoja ili kurahisisha shughuli za uokozi pindi maafa yanapotokea.
Madawa ya kulevya:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kukabiliana na changamoto za Madawa ya kulevya hapa
Zanzibar, Serikali kupitia Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa
Dawa za Kulevya imeweza kuandaa mpango maalum (Road Map)
wa utekelezaji wa Sheria ya Dawa za Kulevya. Pia, Serikali
imeanzisha vikao vya Kamati ya Kitaaluma ya Kupambana na Dawa za Kulevya
na kuandaa Sera ya Dawa za Kulevya na kufanya mikutano na vyombo vya
kusimamia sheria (Law Enforcement Agency- LEA) ili kukuza
mashirikiano na vyombo hivyo kwa kudhibiti mapambano ya Dawa za
Kulevya. Aidha, Serikali imetoa taaluma juu ya madawa ya kulevya katika
maeneo ya
kazi, maskulini, Shehia na makundi mbali mbali Unguja na Pemba.
Pia Serikali imetayarisha muongozo wa nyumba za makaazi ya
vijana walioacha matumizi ya Dawa za Kulevya (Sober House).
Demokrasia na Utawala Bora:
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kusimamia demokrasia na utawala bora nchini, Serikali imeandaa Sera ya Utawala Bora pamoja na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa lengo la kutoa miongozo ya utekelezaji wa demokrasia na utawala bora nchini. Aidha, Serikali imetoa elimu ya uraia kwa wananchi juu ya Sera ya Utawala Bora, Rushwa na Haki za Binaadamu kupitia vyombo vya habari, ziara za vijijini pamoja na kutumia vikundi vya sanaa za maonesho. Pia, Sheria na Kanuni za kuzuia rushwa na uhujumu uchumi zimetayarishwa na kuanza kutumika. Sambamba
na
hilo, Serikali imeiimarisha Mamlaka ya Kuzuia Rushwa kwa kuwasomesha na
kuwapatia mafunzo kwa vitendo watendaji wa Mamlaka hiyo.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kusimamia uwajibikaji na utawala bora kwa watendaji
wa Serikali, Serikali meimarisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali kwa ujenzi wa majengo ya kisasa na
uwekaji wa vifaa vya kisasa vya utunzaji kumbumbu wa kazi za
ukaguzi pamoja na kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na mrefu wafanyakazi
wake katika fani za ukaguzi wa thamani (Value for Money Auditing) kwa
lengo
la kuiwezesha Ofisi hiyo kuimarisha kazi za ukaguzi na kutoa ripoti za
ukaguzi zilizokuwa na viwango inavyokubalika Kimataifa na kwa wakati
muafaka.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali imeendelea kudumisha Muundo wa Serikali ya Umoja
wa Kitaifa kama livyoelekezwa katika Katiba ya Zanzibar kutokana na
mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya 1984
Toleo la 2010. Aidha, Serikali imeendelea kuzingatia na
kudumisha misingi ya kidemokrasia na utawala bora kwa kuhakikisha kuwa
mihimili mikuu mitatu (Mahakama, Serikali, na Baraza la Wawakilishi)
ya demokrasia na utawala bora inafanya kazi zake kwa uhuru bila
ya kuingilia na chombo chengine. Vile vile, Serikali imefanya Mikutano
na
Vikao vyake vyote vya kisheria kwa lengo la kujadili Nyaraka
kadhaa zikiwemo za Sheria, Sera pamoja na kupokea na kujadili taarifa
mbali mbali. Aidha, mikutano mbali mbali kati ya Mheshimiwa Rais
na Viongozi wa Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kujadili utekelezaji wa malengo ya bajeti imefanyika.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kuendeleza elimu hiyo ya muundo mpya wa Serikali
yetu, Serikali imetoa elimu juu ya Mfumo wa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Maafisa Wadhamini,
Maafisa Tawala wa Mikoa na Wilaya pamoja na Wawakilishi wa Jumuiya
za Kiraia Unguja na Pemba. Aidha, Serikali imetoa vipeperushi juu
ya mfumo huo kwa ajili ya kutumika katika kutoa elimu hiyo kwa
makundi mbali mbali ya kijamii. Pia, Viashiria vya Kitaifa vya Utawala
Bora vimeandaliwa na kutumika kwa ajili ya kusimamia uwajibikaji na
ufanisi katika utendaji wa Shughuli za Serikali.
OFISI YA MKURUGENZI WA MASHTAKA:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali imeanzisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka
Zanzibar kwa mujibu wa Sheria ya Kuanzishwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashtaka Nam. 2/2010. Aidha, kitabu cha Muongozo wa Uendeshaji Mashtaka
kimetayarishwa na kutumika. Vile vile, Serikali imejenga jengo jipya
lenye Maktaba ya sheria ya kisasa yenye vitabu mbali mbali vya sheria
ambapo Wafanyakazi na Wanasheria wa Serikali kutoka Taasisi mbali mbali
pamoja na wanafunzi wa Sheria wanaitumia Maktaba hiyo. Aidha, Serikali
imeendelea kuimarisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa kuwajengea
nyumba za makaazi waendesha Mashtaka, kujenga kituo cha Mafunzo ya
Sheria, kufanya matengenezo ya Kitengo cha Uendeshaji wa Mashtaka na
kuwapatia fursa ya kujiendeleza
kielimu watendaji wake.
Kuimarisha Kiwanda cha Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Saba inaendelea na mpango wake wa
kukifufua Kiwanda cha Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ili
kuinua kiwango cha uzalishaji pamoja na kuongeza ubora wa
huduma na bidhaa zinazozalishwa katika kiwanda hicho. Awamu ya Kwanza ya
Mradi/Mpango huu tayari imeshatekelezwa ambapo shughuli zilizofanywa ni
pamoja na kuyafanyia matengenezo makubwa majengo
mawili ya kilichokuwa Kiwanda cha Sigara, Maruhubi kwa ajili ya
kuweza kutumika kuwa Kiwanda cha Idara ya Upigaji Chapa na Mpiga Chapa
Mkuu wa Serikali. Aidha, Serikali imenunua na kufunga mashine za kisasa
za
upigaji chapa (Digital Printing Machines) na kutoa mafunzo ya muda mfupi
ya utumiaji wa mashine hizo kwa watendaji. Kutokana na matengenezo hayo
na uwekaji wa mashine kwa Awamu ya Kwanza, Kiwanda
cha Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali hivi sasa
kinatoa machapisho mbali mbali ya Serikali na sekta binafsi kwa kiwango
bora na kwa wakati.
SERIKALI ZA MITAA NA IDARA MAALUM:
Serikali za mitaa:
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendelea kuziimarisha Serikali za Mitaa, Serikali imefanikiwa kuandaa Sera ya Serikali za Mitaa na kufanikisha kufanya mapitio ya Sheria mbili (Sheria Nam.1 ya 1998 ya Tawala za Mikoa na Sheria Nam. 3 na 4 ya Baraza la Manispaa) na kuwa na Sheria Mpya Namba 8 ya mwaka 2014 ya Tawala za Mikoa na Sheria Namba 7 ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa ya mwaka 2015. Aidha, Serikali imewajengea uwezo wafanyakazi wa Serikali za Mitaa kwa kuwapa mafunzo ya muda mrefu na mfupi pamoja na ziara za kimasomo na kubadilishana uzoefu ndani na nje ya nchi. Pia, elimu juu ya kuanzisha mfumo madhubuti wa ukusanyaji na utunzaji wa mapato ya Serikali za Mitaa (Data base System) katika Taasisi za Halmashauri zote za Unguja na Pemba imetolewa.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za
jamii katika miji ya Zanzibar kupitia Mradi wa Huduma za Jamii Mjini
(Zanzibar Urban Service Project). Kupitia mradi huu uwezo wa kitaasisi
wa Baraza la Manispaa Zanzibar na Mabaraza ya Miji ya Pemba umeimarishwa
kwa kufanya ukarabati wa majengo, kutoa mafunzo kwa wafanyakazi na
ununuzi wa vifaa vya ofisi yakiwemo magari na vifaa vya usafi. Aidha,
Serikali imefanikiwa kuweka mazingira bora ya kazi kwa kujenga Ofisi za
kisasa zinazokidhi mahitaji kwa Taasisi za Halmashauri za Unguja na
Pemba.
Pia katika kutoa huduma kwa wananchi Serikali imekuwa karibu na jamii katika kusaidia miradi ya maendeleo
kwa
kuwahamasisha wananchi kuunda Kamati za Maendeleo za Shehia na Majimbo
ili kusimamia miradi ya maendeleo. Idara/vikosi Maalum vya SMZ:
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jitihada za kuviimarisha vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali imetoa mafunzo ndani na nje ya nchi kwa wapiganaji wa vikosi hivyo katika fani mbali mbali. Pia Serikali imefanya matengenezo ya majengo, utoaji wa vifaa na ukarabati wa miundombinu ya maji na umeme kwa kambi zote za Unguja na Pemba ili kuleta ufanisi zaidi wa utendaji kazi kwa vikosi hivyo.
MFUKO WA HIFADHI YA JAMII:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, Serikali imekamilisha uandaaji wa Sera ya Hifadhi ya Jamii na kuanza utekelezaji wake. Lengo la Sera hiyo ni kujenga mfumo wa hifadhi ya jamii unaolenga kutoa huduma bora za hifadhi kwa watu wote, hasa maskini na wanaoishi katika mazingira magumu zaidi. Aidha, Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii imeanzisha Mfumo wa uchangiaji wa hiari (Zanzibar Voluntary Social Security Scheme) ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na kunufaika na matunda ya
hifadhi ya jamii yanayotolewa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar pia umeweza kuwekeza
katika miradi mbali mbali ya maendeleo, miongoni mwa miradi hiyo ni
ujenzi wa viwanja vya kufurahishia watoto Kariakoo kwa Unguja na
Tibirinzi kwa Pemba, ujenzi wa Mnara wa kumbukumbu ya miaka 50
ya Mapinduzi ya Zanzibar na ujenzi wa nyumba za makaazi. Aidha,
Mfuko umeweza kutoa mikopo kwa Taasisi mbali mbali zikiwemo za Serikali
na binafsi ikiwa ni moja ya njia ya kuwekeza fedha zinazotokana
na michango ya wanachama wa Mfuko kama inavyoelezwa katika Sheria
ya Mfuko ikiongozwa na Sera ya Uwekezaji ya Mfuko.
KUYAENDELEZA MAKUNDI MBALI MBALI:
Watoto:
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika juhudi za kuimarisha maslahi ya watoto wetu, Serikali imeandaa Sheria ya Mtoto ya 2011 na kutengeneza Kanuni 7 za kusimamia utekelezaji wa Sheria hiyo pamoja na uandaaji wa Sera na Mikakati mbali mbali yanayohusiana na hifadhi na maendeleo ya mtoto ambayo yanahusisha masuala ya hifadhi ya mtoto, usajili wa vituo na makaazi ya kulelea watoto, ukaazi na ulezi wa kambo pamoja na kinga maalum kuhusu hifadhi, ridhaa ya kupima Ukimwi na matibabu. Vile vile, Serikali inaendelea kuimarisha Mfumo wa hifadhi ya mtoto ikiwemo
uanzishwaji
wa mahakama za watoto. Aidha, Serikali imesimamia uundwaji wa Mabaraza
ya Watoto nchini kwa lengo la kuwakutanisha watoto kuzungumza masuala
yanayowahusu pamoja na changamoto zinazowakabili.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kuendeleza malezi bora ya watoto, Serikali
imekamilisha ujenzi wa nyumba ya kulelea watoto Mazizini na tayari
watoto wanalelewa katika nyumba hiyo. Serikali pia, imeandaa
na kuisambaza miongozo ya uanzishaji na uendeshaji wa nyumba za
kulelea watoto kwa taasisi binafsi kwa lengo la kuimarisha malezi ya
watoto katika vituo hivyo. Aidha, Serikali imefanya zoezi la kuvitambua
vituo vya kulelea watoto na kusimamia utekelezaji wake. Vile vile,
Serikali inaendelea na usajili wa kuwatambua watoto walio katika
mazingira
magumu kwa Unguja na Pemba.
Wanawake:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika utekelezaji wa Sera ya Hifadhi na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2001, Serikali imeweza kuwajengea uwezo na uthubutu wanawake wa kutumia fursa za kujiendeleza kiuchumi, kijamii na kisiasa. Wanawake wengi hivi sasa wameweza kumiliki mitaji na kufanya biashara kubwa na ndogo zinazoendesha maisha yao, familia zao na kuchangia uchumi wa taifa. Hali hii imetokana na Serikali kuvipatia mafunzo, kuvihamasisha, kuvishauri na kuvitembelea vikundi vya wanawake vya uzalishaji mali, wajasiriamali na SACCOS.
Aidha, wanawake wameweza kujitokeza kugombea nafasi mbali mbali za uongozi ambapo idadi yao imeongezeka katika ngazi ya utoaji wa maamuzi. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji,
Serikali
kwa kushirikiana na Shirika la Action AID imeanzisha nyumba salama kwa
ajili ya kuwahifadhi na kuwahudumia waathirika wa vitendo vya
udhalilishaji. Pia, Serikali imezijengea uwezo Kamati za Kupambana
na Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia kutoka ngazi ya Taifa
hadi Shehia, kuunda mtandao wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji
wa kijinsia, kuandaa miongozo ya kufundishia na kushirikiana na
viongozi wa dini katika mapambano hayo. Aidha, Serikali imefanya
uchambuzi wa sheria na kanuni zinazohusiana na udhibiti wa vitendo
vya udhalilishaji wa kijinsia, ambapo imeweza kubaini mapungufu
mbali mbali na baadhi ya mapungufu hayo tayari yameanza kufanyiwa kazi.
Vijana:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwa lengo la kuwaendeleza vijana, vikundi vya vijana
vimefanyiwa tathmini ya mahitaji na changamoto zao ili kutafuta njia ya
namna ya kuviendeleza vikundi hivyo. Pia, Serikali imekamilisha uandaaji
wa Sheria na Kanuni ya kuanzisha Baraza la Vijana Zanzibar lenye lengo
la kuwashirikisha vijana katika ngazi
mbali mbali za maamuzi. Aidha, Baraza hilo tayari limeshaundwa na Katibu
wa Baraza la Vijana tayari ameshateuliwa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Aidha,
Serikali imezindua mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi
kwa kuiunganisha Mfuko wa Kujitegemea, Mfuko wa AK/JK na Mfuko wa
Vijana ili kuweza kukabiliana na tatizo la ajira na kuinua uchumi
wa Zanzibar. Vile vile, kwa mashirikiano na Taasisi mbali mbali
za Serikali na Binafsi, Serikali imeendelea kuishughulikia changamoto ya
upatikanaji wa ajira hasa kwa vijana nchini kwa kuwaorodhesha
watafuta kazi kupitia Kituo cha Kutoa Taarifa za Soko la Ajira ili
kuweza kuwaunganisha na waajiri. Jumla ya vijana 2,473 wameorodheshwa,
ambapo vijana 1,978 wamefanikiwa kuajiriwa ndani na nje ya nchi
kupitia Kituo hicho.
Wazee:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutoa misaada ya kijamii kwa wazee
wasiojiweza pamoja na kutoa posho la kujikimu wazee wenye watoto
wanaoishi katika mazingira magumu zaidi. Vile vile Serikali inaendelea
na kuihamasisha jamii kuendeleza utamaduni wa kuwaheshimu, kuwaenzi na
kuwatunza wazee wetu. Kila ifikapo siku ya tarehe 01 Oktoba ya kila
mwaka Serikali inasimamia na kuadhimsha siku ya wazee Duniani kwa lengo
la kutathmini mafanikio na changamoto zilijitokeza katika jitihada za
kuwatunza, kuwaheshimu na kuwaenzi wazee hao ikiwa ni pamoja na
kuihamasiha jamii pamoja na wadau wengine kuongeza juhudi za kuendeleza
mikakati hiyo nchini.
Watu Wenye Ulemavu:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, ili kuwa na takwimu sahihi za Watu Wenye Ulemavu na aina ya
ulemavu walionao pamoja na kurahisisha upangaji wa Sera, Mikakati ya
Mipango mbali mbali hapa nchini, Serikali imefanya usajili katika Wilaya
zote za Unguja na Pemba katika ngazi ya Shehia.
Vile
vile Serikali imeendelea kutoa elimu inayohusu mikataba, haki, fursa na
wajibu wa Watu Wenye Ulemavu katika Mikoa ya Unguja na Pemba. Serikali
imetoa ruzuku na visaidizi kwa Jumuiya za Watu Wenye Ulemavu
ili ziweze kutimiza malengo yao.
Wafanyakazi:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwa upande wa wafanyakazi Serikali imefanya mapitio ya
Sheria za Kazi, imetayarisha na kusambaza Kanuni za Sheria ya Ajira
Nambari 11 ya mwaka 2005 na Kanuni za Utumishi wa Umma kwa wahusika
wote. Kanuni hizo zinahusu mambo mbali mbali yakiwemo maslahi ya
wafanyakazi katika sekta binafsi, usajili na utendaji kazi wa Vyama vya
wafanyakazi, mikataba, likizo bila ya malipo na makundi
maalum ya wafanyakazi.
SEKTA YA SHERIA:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kuimarisha sekta ya sheria, Ilani ya CCM mwaka
2010-2015 imeagiza Serikali kuimarisha Mahakama kwa kujenga majengo
mapya, kuzipatia vifaa vya kisasa, kujenga nyumba za Mahakimu
Unguja na Pemba na kufanya marekebisho ya Sheria na Kanuni za
Utendaji kazi wa Mahakama. Katika kulitekeleza agizo hilo, Serikali
imefanya matengenezo makubwa ya majengo ya Mahakama na kuziwekea
vitendea kazi kwa Unguja na Pemba. Aidha, Serikali imeanzisha Kitengo
kinachohusiana na masuala ya Mikataba, ambacho kina wataalamu
wanaoshughulikia masuala yote ya mikataba ya Serikali.
Pia, Serikali imewapatia mafunzo maafisa wa Sheria kutoka Taasisi mbali mbali juu ya uandishi wa
sheria,
utatuzi wa migogoro, ufungaji na uingiaji wa mikataba ya kitaifa na
kimataifa. Mafunzo hayo yamedhaminiwa na Serikali kwa mashirikiano na
UNDP kupitia Mradi wa Mageuzi katika Sekta ya Sheria (Zanzibar legal
Sector Reform Program).
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kupunguza mrundikano wa kesi Mahakamani, Serikali
imeajiri Mahakimu wapya na imeanzisha Kamati ya kusukuma kesi kwa
kuwashirikisha wadau wote wa masuala ya kesi. Vile vile, Mahakama
kupitia Mradi wa Mageuzi ya Sekta ya Sheria inaendelea na utaratibu
wa kuanzisha mfumo wa kisasa wa usimamizi wa uendeshaji kesi
(Case Management System).
Aidha,
Serikali kupitia Programu ya Mabadiliko katika Sekta ya
Sheria, imewapatia mafunzo Majaji, Mahakimu na waendesha mashtaka
ili kuwazidishia ujuzi katika utendaji wa kazi zao za kila siku.
Aidha, Serikali imepeleka huduma za Mahakama karibu na wananchi kwa
kuendesha vipindi vya redio na televisheni, mikutano ya hadhara katika
Shehia na maskuli na kutoa na kusambaza kwa wananchi matoleo mbali mbali
ya Jarida la Mahakama la Shahidi kwa ajili ya kuelimisha wananchi
kuhusu huduma na masuala ya mahakama na jinai.
CHANGAMOTO ZILIZOATHIRI UTEKELEZAJI WA ILANI:~
Mheshimiwa
Mwenyekiti, pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 hadi 2015,
kulijitokeza baadhi ya changamoto ambazo Serikali ililazimika kutumia
rasilimali zake chache ili kukabiliana nazo. Changamoto hizo ni pamoja
na kutokea kwa vitendo au matukio yaliyoashiria uvunjifu wa amani,
kutokea kwa maafa mbali mbali, ikiwemo kuzama kwa Meli ya Spice Islander
huko eneo la bahari ya Nungwi na Meli ya MV Skagit katika maeneo ya
Chumbe ambapo zaidi ya watu 1,600 walipoteza maisha.
Changamoto
nyengine ni kutokea kwa upepo mkali katika maeneo mbali mbali ya visiwa
vya Unguja na Pemba na kuleta uharibifu wa makaazi ya watu na mazao.
Majanga haya yalipelekea kupoteza kwa nguvu kazi pamoja na matumizi
makubwa kwa Serikali ambayo hayakutarajiwa. Aidha, Mfumko wa bei za
vyakula uliotokana na tatizo la kupanda bei za mafuta na chakula katika
soko la dunia, hasa katika miaka ya 2010 na 2011.
Wananchi
wengi hasa wenye kipato cha chini waliathirika na tatizo hilo kwa
kushindwa kununua chakula na mahitaji yao mengine ya msingi.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbali
mbali walikabiliana na majanga hayo kwa pamoja, ikiwemo huduma za uokozi
na huduma za kibinaadamu na kutoa pole kwa waathirika. Kwa upande wa
mfumko wa bei, Serikali ilihamasisha wananchi hasa wakulima
kuongeza bidii katika shughuli za kilimo na uzalishaji mali ili kuweza
kupata chakula cha uhakika na kujiongezea kipato pamoja kutoa ruzuku
katika pembejeo na matrekta katika kilimo na ushuru wa bidhaa za
chakula zinazoingizwa nchini ili kudhibiti mfumko wa bei.
HITIMISHO:
Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwa ujumla katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2010 -
2015), Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitekeleza maagizo ya Ilani ya
Uchaguzi ya CCM kwa mafanikio makubwa ya wastani wa kiwango cha asilimia
90. Mafanikio haya kwa kiasi kikubwa yametokana na mashirikiano na
mshikamano kati ya wananchi na viongozi katika ngazi mbali mbali katika
jamii yetu kuanzia ngazi ya Shehia, Wilaya, Mkoa hadi Taifa. Kutokana na
mafanikio yaliyopatikana ni dhahiri kwamba wananchi wameongeza imani ya
Chama cha Mapinduzi na watakichagua tena kuongoza Serikali zote mbili
(2) kwa kishindo kikubwa katika Uchaguzi utakaofanyika mwezi Oktoba,
2015.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, nachukua fursa hii kutoa shukrani zangu kwa Sekta Binafsi,
Asasi za Kiraia, Washirika wa Maendeleo na nchi marafiki kwa ushirikiano
na mahusiano yao yaliyoiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake kwa
ufanisi mkubwa sana. Tunaomba mashirikiano hayo yaendelee ili kuleta
maendeleo ya kudumu katika nchi
yetu na kuwaondoshea wananchi wetu umasikini.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwa mara nyengine tena napenda kutoa shukrani zangu za
dhati kwako, kwa Wajumbe wote wa Kamati Kuu ya CCM pamoja na waalikwa
wote. Nawashukuru wote kwa kunisikiliza kwa makini.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
Naomba kuwasilisha.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
No comments:
Post a Comment