Wednesday, November 18

Toka Ufaransa...Polisi wavamia washukiwa wa mashambulio Paris...


Washukiwa wawili wamefariki baada ya maafisa wa usalama kushambulia Saint Denis kaskazini mwa Paris, wakisaka waliohusika mashambulio ya Ijumaa.
Ufyatulianaji mkali wa risasi umetokea mapema asubuhi kwenye mtaa huo. Operesheni hiyo inadaiwa kumlenga mwanamgambo wa Islamic State Abdelhamid Abaaoud ambaye amedaiwa kupanga mashambulio hayo yaliyoua watu 129.
Maafisa kadha wa polisi wamejeruhiwa kwenye operesheni hiyo, kituo cha runinga cha BFMTV cha Ufaransa kimeripoti.
Video iliyoonyeshwa na vituo vya televisheni vya BFMTV na iTele zimeonyesha watu walioshuhudia wakisema milio ya risasi ilianza kusikika saa kumi unusu alfajiri saa za Ufaransa.
Naibu meya Stephane Peu amewahimiza raia wasalie manyumbani, akisema "hili si shambulio jipya bali ni operesheni ya polisi".

Awali, duru za kiusalama zilisema video ya kiusalama ilikuwa imeonyesha huenda kulikuwa na mshambuliaji wa tisa mashambulio hayo ya Ijumaa.
Watu 129 walifariki kwenye mashambulio yaliyotokea maeneo sita mjini Paris.
Kundi la Islamic State (IS) limesema ndilo lililotekeleza mashambulio hayo.
Ripoti moja inasema barabara zimefungwa eneo la Place Jean Jaures mtaa wa Saint Denis.
Uwanja wa taifa wa michezo wa Stade de France, ambako washambuliaji walilipua mabomu Ijumaa, umo kwenye mtaa huo.

No comments: