Aliyekuwa Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola,
amethibitisha kuwa kwenye mazungumzo na Klabu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC FC)
inayoshiriki Ligi Darala la Kwanza, lakini hofu imetanda klabuni hapo, kwani
imebainika haziivi na kocha wa timu hiyo, Amri Said ‘Jap Stam’ ambaye pia
aliwahi kuwa kwenye benchi la Simba msimu wa 2010.
Matola ambaye aliachana na Simba wiki iliyopita kwa
kile alichobainisha ni kutokuwa na maelewano mazuri na kocha mkuu, Dylan Kerr,
amesema amefanya mazungumzo na uongozi wa klabu ya KMC FC, lakini bado
hawajafikia muafaka.
“Wao walinifuata tukazungumza kiutendaji lakini
hakukuwa na muafaka katika mazungumzo yetu. Kama tutamalizana vizuri taarifa
zitatolewa tu na siyo jambo la kuficha,” alisema Matola.
Hata hivyo, kuonyesha kuwa uhusiano wake na Matola
siyo mzuri, Stam alipoulizwa kuhusu Matola kukaribia kujiunga na timu hiyo,
alisema:
“Sijaambiwa chochote kuhusu kumtaka Matola ingawa
taarifa hizo ninazo, kuwa wanataka tusaidiane kuhakikisha tunaipandisha timu
ligi kuu. Nafikiri hilo siyo jukumu lao ni jukumu la kocha mkuu, hivyo walikuwa
na kila sababu ya kunifuata kuniuliza kuhusu mtu sahihi katika kusaidiana
katika harakati hizi.
“Timu inafanya vema na dhamira yangu kuu ni kuipandisha
ligi kuu, hivyo kama ni masuala haya, wanataka kutibua hali ya mambo. Mimi
ndiye ninatakiwa kumtafuta msaidizi wangu na siyo mtu yeyote, maana mimi ndiye
kocha mkuu,” alifunguka kocha huyo aliyewahi pia kuzifundisha Mwadui na Ndanda.
No comments:
Post a Comment